INAWEZEKANA
kabisa kama mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana
Samatta angekuwa hana uvumilivu na nidhamu ya hali ya juu pengine leo hii ndoto
yake ya kwenda Ulaya ingekuwa ishaota mbawa.
Inahitaji
uvumilivu na kuamini zaidi katika ndoto zako ili kuweza kukifanya kile ambacho Samatta
ameweza kukifanya hadi kutua England na kujiunga na Klabu ya Aston Villa ambayo
inashiriki Premier League.
Samatta
ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Premier, ligi kubwa yenye
umaarufu kemkem, hakuna asiyependa kucheza hapo. Tanzania tunajivunia yeye.
Lakini yote
tisa kumi, nidhamu, kijana alikuwa na nidhamu ya hali ya juu tangu yuko
Simba kisha akaenda TP Mazembe hapo akapanda ndege tena kwenda kujiunga na KRC
Genk ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Sasa hivi
yuko sehemu yenye baridi, England katika mji wa Birmingham, kwa sasa kuna
baridi kali sana. Barafu limetanda juu ya nyumba za watu. Hapana shida Samatta
anaweza kuvumilia maana akiangalia alikotoKa hasira za kusonga mbele zaidi
zinamjia.
Sasa hiki
ndicho kitu ambacho wachezaji wengine wengi wa Bongo wanakikosa. Uvumilivu
hawana. Imewahi kutokea kuna mchezaji fulani aliwahi kwenda kufanya majaribio
nje ya nchi na akafanya vyema tu akiwa kwenye hatua za kujadiliana masuala ya
mkataba fasta akarudishwa nyumbani ili acheze mechi ya watani.
Inasikitisha
sana. Samatta sasa kaonyesha njia. Kubalini kuifuata licha ya kuwa ina mabonde,
milima na vikwazo vingine mbalimbali. Ninyi vijana mnaochipukia hakikisheni mnafuata
nyayo za Samagoal hakika mtafanikiwa.
Samatta
amekuwa ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wa Tanzania kutokana na uvumilivu na
nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja jambo ambalo kimsingi limemjenga
na kumfikisha hapo alipo sasa.
Safari ya
kuelekea mafanikio kama aliyonayo Samatta inahitaji moyo wa uvumilivu, nidhamu
na kutokubali kurudi nyuma hata kama safari hiyo ina vigingi na miba ndani
yake.
Wengi
wameenda kama alivyoondoka Samatta lakini mwisho wa siku tumekuwa tukishuhudia
wakirudi kimyakimya na visingizio rundo, ambavyo asilimia kubwa vimekuwa havina
mbele wala nyuma.
Waliobahatika
kwenda Ulaya hawakudumu kwa kisingizio cha baridi kali au chakula kibaya!
Walirudi nchini kwa sababu zisizoeleweka kutokana na kushindwa kuvumilia maisha
ya ughaibuni.
Ule uhuru
ambao walikuwa wameuzoea wa kwenda katika vijiwe vya Sinza, Temeke, Ilala au
wale mabinti ambao wamezoea kila baada ya kutoka mazoezi au mechi ‘kujivinjari’
nao huko Ulaya hawapatikani kwa urahisi.
Sasa kwa
kuwa Samatta katangulia Ulaya basi awe kama somo kwenu, msomeni, msimiss mihogo
na chips za Sinza kwani zipo miaka yote, ninyi pambaneni kwanza na maisha na
kuitangaza nchi yetu kimataifa.
Sasa mbele
ya runinga tunamuangalia Samagoal akicheza mechi kwenye Premier League na mechi
yake ya kwanza mbele ya Bournemouth pale Uwanja wa Dean Court, alitupia
ikifikia mwakani basi tuwe tunakaa kuangalia mechi za Watanzania wengine
wakicheza La Liga, Bundesliga, Serie A au hata Ligue 1.
0 COMMENTS:
Post a Comment