JUMAPILI hii. Machi 8 kutakuwa na mechi ya watani wa jadi kutoka Jiji la Manchester pale England ambapo wenyeji Manchester United watawaalika Manchester City.
Mchezo huo wa Manchester Derby unaotarajiwa kuchezwa kuanzia saa 1:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, utachezwa kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Mpaka sasa, rekodi zinaonyesha kuwa, timu hizo zimekutana mara 181 katika michuano yote, Man United imeshinda 75, Man City 54, huku sare zikiwa 52.
Kwa msimu huu, timu hizo zinakutana kwa mara ya nne. Man United imeshinda mara tatu na Man City mara moja. Hivyo mchezo huu wa Jumapili moto utawaka. Man United inataka kushinda mechi ya tatu na Man City inataka kuweka mzani sawa.
Katika msimamo wa Premier, Man United inashika nafasi ya tano na Man City ya pili.
Wakati tukielekea kushuhudia mchezo huo, mwamuzi ameshatambulika ambaye ni Mike Dean, huku mashabiki wa Manchester United wakianza kuingiwa na hofu.
Dean atakuwa akichezesha Manchester derby ya sita katika maisha yake ya kuchezesha soka.
Katika mechi hizo zote, Man City imeshinda tano, huku moja pekee wakipoteza. Jambo hilo linatafsiriwa na mashabiki wa Man United kwamba wanakwenda kupoteza tena.
Imeshuhudiwa katika mechi hizo, Dean ametoa kadi za njano 25 na nyekundu moja kwa Paul Scholes mwaka 2011.
Kwa jumla, Dean ameichezesha Man City mechi 73, huku Man United ikiwa mechi 71. Cha kufurahisha ni kwamba, katika mechi hizo, timu zote zimeshinda mechi 38.
Jumapili hii Dean atasaidiwa na Darren Cann na Dan Robathan, huku mwamuzi wa akiba akiwa Anthony Taylor.








0 COMMENTS:
Post a Comment