March 22, 2020



JANUARI mwaka huu, Mbwana Samatta aliandika historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya Engalnd maarufu kama Premier baada ya kusajiliwa na Klabu ya Aston Villa.
                               
Ni dhahiri kuwa Kocha wa Aston Villa, Dean Smith aliona mbali sana kwa kuamua kumvuta Samatta kutoka KRC Genk ya Ubelgiji kutokana na ubora alionao mshambuliaji huyo raia wa Tanzania.

Ujio wa Samatta ndani ya Aston Villa unaweza kuwa na faida au hasara kwa timu hiyo wakati huu ikiwa katika harakati za kujiokoa na janga la kushuka daraja.

Kwa sasa Premier imesimama kutokana na tahadhari ya maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo vimesababisha mikusanyiko yote inayohusisha watu wengi kupigwa marufuku ikiwemo michezo.

Mpaka Premier inasimamishwa kwenye, Aston Villa ipo nafasi ya 19 ikiwa imekusanya alama 25 tu katika mechi 28.

Kutokana na Aston Villa kuyumba na kuwa mguu ndani mguu nje kwenye Premier, kuna baadhi ya timu zinaonekana kummezea mate Samatta huku ikitajwa kuwa huenda staa huyo mwisho wa msimu huu akaondoka kikosini hapo.

Kuna timu zimetajwa kwamba huenda ndipo Samatta akatua huko. Timu zenyewe hizi hapa;

Tottenham
Kwa miaka mingi, Tottenham maarufu Spurs imekuwa ikimtegemea zaidi Harry Kane katika ufungaji, hili limeonekana kuwagharimu sana msimu huu baada ya staa huyo kuwa majeruhi kwa kipindi kirefu.

Kane ndiyo namba tisa pekee ambaye walikuwa wakimtegemea na baada ya kuumia ikabidi Kocha Jose Mourinho kuamua kumtumia Heung-min Son ambaye naye akapata majeraha.

Lucas Moura sio straika, lakini yupo Troy Parrott ambaye naye anaonekana bado hayupo sawa, hivyo hapa unaiona nafasi ya Samatta iko wazi kabisa kwenda kuwa mbadala sahihi wa Kane.

Crystal Palace
Akiwa Genk, iliwahi kutajwa kuwa Crystal Palace inamuwinda Samatta. Msimu huu Crystal Palace msimu huu wameonekana kuwa na mastraika ambao hawana muendelezo mzuri.

Mfano mzuri ni Christian Benteke ambaye amekuwa hana jipya kutokana na kugubikwa na ukame wa mabao tangu msimu uliopita, Jordan Ayew licha ya kufunga mabao nane, lakini ni straika ambaye pia hana muendelezo mzuri katika kufunga.

Ukija kwa upande wa Wilfred Zaha yeye ni winga na licha ya kupambana hatakiwi kutegemewa peke yake katika kufunga kwa sababu si mshambuliaji halisi.

Kocha Roy Hodgson anapambana kuhakikisha anaondokana na tatizo la ukame wa mabao kwenye kikosi chake na ndio maana alimchukua kwa mkopo, Mturuki, Cenk Tosun kutoka Everton, lakini bado hajapata anachotaka.

Kama Tosun hatapata nafasi ya kusajiliwa moja kwa moja basi, Samatta anaweza kuwa suluhisho la ufungaji ndani ya timu hiyo.

Chelsea
Tayari Kocha Frank Lampard ana Tammy Abraham, Michy Batshuayi na Oliver Giroud katika kikosi chake cha Chelsea, ukiona hivyo unaweza kudhani kocha hana wazo la kusajili straika mwingine.

Kwa msimu huu, Abraham tu ambaye anaonekana yuko juu kwa kufunga mabao, Batshuayi alianza vizuri, lakini bado anaonekana kutomshawishi Lampard, Giroud alionekana kuwa wamoto kabla ya ligi kusimama. Mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Licha ya Abraham kufunga mabao 13 mpaka sasa, lakini Lampard atahitaji kuongeza nguvu kwa kuleta straika mwingine na jicho lake linaweza kumuangalia Samatta licha ya sasa kuripotiwa kuwa wanamfuatilia Moussa Dembele wa Lyon.

Everton
Dominic Calvert-Lewin amefunga mabao 13 kwenye Premier msimu huu, kwa mfumo anaoutumia Kocha wa Everton, Carlo Ancelotti ambao ni 4-4-2, mshambuliaji huyo kwa sasa anachezeshwa na Richarlison wakati huu ambapo Oumar Niasse akishindwa kuonyesha cheche zake.

Kama Villa itashuka daraja, basi Everton watakuwa na nafasi ya kumsajili Samatta na endapo atachezeshwa na Calvert-Lewin na Richarlison itakuwa bonge la kombinesheni kwa kocha Ancelotti.

Arsenal
Wengi wanaweza kushangaa inawezekanaje wakati huu Samatta kukipiga Arsenal, lakini sikiliza hii; Pierre-Emerick Aubameyang mkataba wake unamalizika msimu ujao na kuna uwezekano akaondoka, Alexander Lacazette msimu huu kiwango chake bado sio cha kuridhisha.

Gabriel Martinelli na Eddie Nketiah bado ni makinda ambao Kocha Mikel Arteta anawaandaa, hivyo kama wakifanya chaguo la kumsajili Samatta itakuwa sahihi kutokana na ufinyu wa bajeti yao.

3 COMMENTS:

  1. Unajifariji tu...wala hakuna timu ya kumnunua yy ateremke daraja tu

    ReplyDelete
  2. Anataka kutufanya wajinga wakati hakuna hata timu moja iliyoonyesha nia

    ReplyDelete
  3. Du wabongo kwa kuwa madalali hatujambo. Sa samatta amefanya nini kimya hapo hadi aende spurs, asenal na chelsea. Acheni kupromo vitu vya uongo

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic