KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael amepanga kushusha kiungo mmoja mkabaji wa kimataifa atakayecheza namba sita baada ya kugundua upungufu katika safu hiyo.
Safu hiyo ya kiungo hivi sasa inachezwa na Mkongomani, Papy Tshishimbi na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambao kocha ameonekana akiwatumia katika michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA msimu huu.
Kati ya viungo wanaotajwa kutua Yanga ni kiungo wa Nkana Rangers ya Zambia, Musa Mohamed ambaye mwenyewe alithibitisha kupitia kwenye moja ya mtandao wa nchini humo kuwa yupo kwenye mazungumzo na Yanga iliyoonyesha nia ya kumsajili.
Eymael amesema kuwa anaamini uwezo wa viungo alionao Yanga, lakini ni lazima asajili kiungo mmoja anayeimudu vema nafasi hiyo ya kiungo huyo atakayeanzisha mashambulizi kuanzia chini kwenda juu.
“Msingi wa timu siku zote unaanzia chini, nikimaanisha namba sita ambaye kama yeye akishindwa kutimiza majukumu yake vizuri, basi lazima makosa yatakuwa mengi golini kwetu.
“Kama umekuwa ukifuatilia mechi ambazo tumekuwa tukipoteza makosa mengi yamekuwa yakifanywa na viungo wakabaji namba sita wamekuwa hawatimizi vema majukumu yao ya uwanjani.
“Hivyo, basi nimepanga kusajili kiungo mkabaji mmoja mwenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi hiyo ya kiungo ambaye hatakuwa akihama katika eneo lake la katikati, tayari nipo kwenye mazungumzo na baadhi yao kutoka mataifa mbalimbali ambayo nisingependa kuweka wazi kwa hivi sasa,” amesema Eymael.
Chanzo Championi
0 COMMENTS:
Post a Comment