KINACHOSUBIRIWA kwa sasa ni muda tu wa kuanza mahesabu ya kile ambacho wachezaji walikuwa wamepanda wakati ule masuala ya michezo yalipokuwa yamesimamishwa kwa muda.
Ikumbukwe kwamba Machi 17 masuala yote ya michezo yalisimamishwa na Serikali ya Tanzania kutokana na kuibuka kwa janga la Virusi vya Corona ambalo linaivurugavuruga dunia namna linavyotaka.
Haikuwa Tanzania pekee bali dunia nzima ilikuwa kwenye janga la ukiwa ikipambana kutafuta suluhisho la kusambaa kwa janga hilo ambalo bado lipo.
Tayari tunaona Serikali imeruhusu kuanza kwa michezo huku ikizitaka mamlaka za michezo kuendelea kusimamia michezo na kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona.
Kwa kuwa mamlaka husika imeruhusu mechi kuanza hilo ni jambo jema ambalo wadau wa michezo wamefurahia kuona mambo ambayo tuliyakosa muda mrefu yanarejea.
Kinachotakiwa kwa sasa ni maandalizi mazuri kwa kila timu ili kupata matokeo ya kile ambacho walikuwa wanakitafuta kabla ya ligi kusimamishwa.
Ninaamini kuwa kila mmoja ambaye anapenda michezo atakuwa anafurahi kuona kwamba yale aliyokuwa akiyakosa muda mrefu yanarejea tena.
Burudani ya soka haikuonekana kwa muda wa miezi miwili sio kitu cha kubeza ni muda mrefu ila kwa kuwa ilikuwa ni dharula hakuna namna ni lazima kila mmoja akubali hali halisi .
Hakuna namna ya kufanya zaidi ya kutafuta njia ya kutoka hapa tulipo kwa kuendelea kuchukua tahadhari muhimu dhidi ya Virusi vya Corona.
Kurejea kwa ligi kutukumbushe kwamba ni lazima kila mmoja aendelee kuchukua tahadhari zaidi yasije yakatokea maambukizi zaidi yatakayofanya burudani kusimamishwa tena.
Wachezaji ni wakati wao wa kuonyesha kwamba walikuwa na nidhamu binafsi kwa kutekeleza program ambazo walipewa.
Kitakachowaonyesha kwamba walikuwa na nidhamu ni uwezo wao ndani ya uwanja kwa kupambana kwa hali na mali kupata matokeo.
Wale ambao walikuwa wakitegea muda wao wa kuonekana umewadia kwani hakutakuwa na muda wa kujificha kila kitu kinakuwa hadharani.
Juni 13 ligi inatarajiwa kuanza kutimua vumbi na kwa muda ambao haikuchezwa mambo yatakuwa magumu kwa mchezaji ambaye alikuwa anapuuzia.
Zipo zile ambazo wakati ligi inasimamishwa zilikuwa kwenye nafasi ya kushuka Daraja la Kwanza ,(Fdl)
Kwa zile ambazo zipo kwenye hatari ya kubwa ya kushuka daraja lazima zipambane kupata matokeo mazuri.
Hii ni lala salama kila timu inahaha kupata ushindi kwa namna yoyote ndani ya uwanja hakuna muda wa kupoteza.
Hili na liwe kwa timu zote kwani mashabiki wanahitaji kuona wanafurahi na ili wafurahi ni lazima timu ishinde.
Katika kucheza ndani ya uwanja ni lazima kila mmoja atambue kuwa Corona bado ipo tahadhari muhimu ikichukuliwa kila wakati.
0 COMMENTS:
Post a Comment