ADAM Oseja, kipa namba mbili wa Namungo FC amesema kuwa kikubwa ambacho kinaibeba timu hiyo ni ushirikiano pamoja na jitihada za wachezaji kupambana ndani ya uwanja.
Oseja alikuwa kipa namba moja wakati Namungo ikipanda daraja kushiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20, kwa sasa kipa namba moja ndani ya Namungo ni Nurdin Barola.
Namungo inayonolewa na Hitimana Thiery, jana ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Mabatini.
Leo wameanza safari kurejea makao makuu ya timu, Lindi ambapo wana mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali dhidi ya Alliance utakaopigwa Uwanja wa Majaliwa.
Akizungumza na Saleh Jembe, Oseja amesema kuwa kila mmoja anacheza kwa juhudi kusaka matokeo ndani ya uwanja ili kufikia malengo waliyojiwekea.
"Kila mmoja anacheza kwa juhudi na ushirikiano ambao tunao ni mkubwa jambo ambalo linatufanya tupate matokeo chanya kwenye mechi zetu licha ya changamoto ndogondogo ambazo zinatokea ni kawaida.
"Kuhusu kuanza kikosi cha kwanza ni jukumu la kocha kwani yeye ndiye anajua nani aanze na pale ambapo ninapata nafasi huwa natimiza majukumu yangu na mwenzangu pia anatimiza majukumu ya timu vizuri," amesema.
Namungo ipo nafasi ya nne ikiwa imecheza mechi 32 kibindoni ina pointi 56.
0 COMMENTS:
Post a Comment