LEO majira ya saa 10:00 jioni, Uwanja wa Uhuru kutakuwa na pambano la kukata na shoka kati ya Yanga na KMC ikiwa ni mchezo wa kirafiki.
Mchezo wa leo ni maalumu kwa timu zote kuangalia utimamu wa wachezaji wao baada ya kukaa tangu Machi 17 bila mechi ya ushindani baada ya Serikali kusimamisha masuala ya michezo kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Miongoni mwa vitu ambavyo mashabiki wamekumbushwa kufanya ni kuvaa barakoa pamoja na kuzingatia umbali wa kukaa mita moja kwa kila shabiki.
Licha ya Serikali kuruhusu masuala ya michezo kuendelea pamoja na mashabiki kufika uwanjani imesisistiza kuwa ni lazima kila mdau kuchukua tahadhari kwani Corona ipo.
Farouk Shikalo mlinda mlango wa Yanga amesema kuwa wapo tayari kuendelea kupambana huku wakizingatia tahadhari za kujilinda.
Hassan Kabunda, winga wa KMC amesema kuwa maandalizi kwao yapo vizuri na bado wanaendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
Mchezo wa leo utakuwa wa tatu kwa Yanga baada ya kuanza na Transit Camp na kushinda mabao 3-1 kisha kazi jana ilikuwa mbele ya Dar City ambapo walishinda mabao 2-0 na leo ni zamu ya KMC.
Mbio za sakafuni. Punguzeni majisifu
ReplyDelete