August 31, 2020


LEO Agosti 31 ni siku ya mwisho kwa timu kukamilisha masuala ya usajili kwa wachezaji wao itakapofika saa 5:59 ukurasa wa usajili unafungwa rasmi.

Sokoni kila timu inapambana kwa masuala ya usajili na tunaona kwamba bado zipo timu ambazo hazijatambulisha wachezaji wao ina maana kwamba bado wapo sokoni kusaka aina ya wachezaji wanaowahitaji.

Usajili sio kitu cha kukurupuka kinahitaji umakini. Muda bado upo basi ninaweza kusema tusubiri na tuone kwa wale ambao wapo kwenye mazungumzo na timu ambazo zinahitaji saini zao.

Pia zipo ambazo zimeshamaliza masuala ya usajili baada ya kuwatambulisha wachezaji pamoja na benchi la ufundi wanastahili pongezi kwa kuwa wameonyesha  walijipanga na wapo tayari kwa ajili ya msimu mpya.

Msimu mpya unatarajiwa kuanza Septemba 6, siku zinakwenda kasi hivyo kwa wale ambao wanadhani ni muda mrefu umebeki wanapaswa washtuke mapema.

Azam, Simba na Namungo hizi hapa tayari zimekamilisha masuala ya usajili na wachezaji wanaendelea na kambi kwa pamoja wakiwa wameshamaliza majukumu yao ya usajili.

Kagera Sugar nao pia wamekamilisha usajili wao kwa kuboresha kikosi chao na kuwapa taarifa mapema wachezaji ambao hawatakuwa ndani ya kikosi hicho.

Ruvu Shooting nao waliwaacha wachezaji kadhaa na taarifa zao ilikuwa ni mapema kama ilivyokuwa kwa Yanga hili pia nalo linastahili pongezi kwani kuwapa wachezaji taarifa mapema inawapa nafasi ya kutambua kwamba wanapaswa wafanye jambo gani.

Kwa zile ambazo hazijafanya hivyo ni muhimu kumalizana na wachezaji wao ili wajue hatma yao.Hakuna muda mwingine ambao watakuwa nao wa kuanza kutafuta timu, dirisha la usajili linakaribia kufungwa.

Kitu pekee ambacho kinatakiwa kufanywa kwa sasa ni kumaliza masuala ya usajili kwa wakati ili kupata muda wa kutengeneza timu kwa ajili ya msimu ujao ambao ninaamini utakuwa na ushindani.

Ninapenda kutoka pongezi kwa timu ambazo zimefanya utambulisho wa wachezaji kwa kuwa kila shabiki alikuwa na furaha ya kuona kile ambacho kimetokea.

Simba, Azam FC hawa walifanya jambo zuri ambalo linastahili pongezi kwa kuwa kila mmoja alikuwa akitimiza jambo lake kwa wakati.

Azam FC kwa mara ya kwanza wao walikuja na Azam Festival na lilijibu kwa kuwa tulishuhudia mashabiki wengi wakijitokeza na kushuhudia burudani ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

Kila mmoja aliona na kila shabiki aliona namna ambavyo mashabiki wanapenda burudani na kushuhudia burudani kutoka kwa wachezaji pamoja na wasanii ambao walipata nafasi ya kutoa burudani.

Simba nao pia jambo lao pia walikuwa na mwendelzo mzuri kwa kuwa mpangilio na ubunifu umeendelea kuonekana kitu ambacho kimewapa furaha mashabiki wao.

Wakati ujao pia tunaamini kwamba maboresho yatakuwepo hasa kwenye mapungufu ambayo yalijitokeza. Kwenye masuala ya upatikanaji wa tiketi awali pamoja na mambo mengine ya kiufundi ni sehemu ambazo zinahitaji maboresho.

Timu ya Namungo pia licha ya kwamba haijafanya tamasha ila tayari mashabiki wameanza kupata picha ya kikosi cha timu yao ambacho kitafanya kazi msimu ujao kwenye ligi na michuano ya kimataifa.

Kwa wale ambao bado hawajatambulisha wachezaji wao muda uliobakia ni sasa ligi itakapoanza gia ya kwanza inabadilika inavutwa nyingine kwa kasi.

Ngoja niongee na wachezaji ambao bado hawajapata timu na wapo kwenye mazungumzo na timu zinazohitaji saini yake.

Kwenda kwenye timu mpya ni furaha ya kila mchezaji ikiwa anakwenda kwenye timu ambayo ina maslahi mazuri lakini kuna ulazima wa kutazama nafasi yake kabla ya kuchekelea kupokea fedha nyingi.

Kwa wachezaji ambao wanahitajika kujiunga na timu nyingine wanapaswa wasikurupuke kwa kuwa nafasi yao ni kuwa wachezaji ndani ya timu ambazo wanakwenda kucheza.

Jambo la msingi ambalo wanatakiwa kuliangalia kabla ya kusaini dili jipya kwa ajili ya wakati ujao ni kutazama nafasi ya kucheza.

Unakwenda kwenye timu kufanya nini pia ni swali ambalo lazima mchezaji ajiulize kwa wakati huu wa usajili kwani wapo ambao wanakwenda kwenye timu na hawajui wanakwenda kufanya nini zaidi ya kufikiria fedha.

Kama unakwenda kwenye timu ukiwa na malengo ya kucheza ili kuendeleza kipaji chako basi ni lazima utazame namna mpya na mtindo mpya wa maisha yako.

Pia lazima utazame timu unayokwenda kucheza kwa nafasi ambayo unacheza kuna nani ambaye anacheza na unaweza kumudu ushindani katika namba hiyo.

Kama hupati nafasi achana na nafasi hiyo tazama maisha yako hapo ulipo. Wakati unakuja, sio lazima kusaini timu ambayo hauna nafasi ya kucheza,mafanikio ya mchezaji yapo kwenye kucheza ndani ya uwanja.

Kama unakwenda kwenye timu ina wachezaji wanne ama watano katika nafasi yako na wewe unakubali kwenda ina maana umekubali kuingia kwenye vita ambayo ukiishindwa muda wako wa kuwa uwanjani unayeyuka kwa msimu mzima ambao utakuwa hapo.

Kinachotakiwa ni kuangalia pia wakati ujao nafasi yako kwenye timu mpya ipoje? Hakuna mchezaji anayeweza kufanikiwa ikiwa atatumia muda mwingi akiwa anasugua benchi.

Muhimu kujifunza pia kwa wachezaji ambao walikuwa wana nafasi ndani ya timu ambazo walitoka na mwisho wa siku walipohama hawakuwa na maisha mazuri kwenye kikosi cha kwanza zaidi wakaishia kusugua benchi.

Nafasi ngumu na inayoua kipaji cha mchezaji kwenye maisha ya soka ni kusugua benchi hasa kwa muda mrefu inamfanya mchezaji apoteze hali ya kujiamini wakati mwingine atakapopata nafasi.

Chaguo ni la mchezaji mwenyewe kwa sasa kwani timu ikiwa inakuhitaji kwa namna moja ama nyingine itatumia nguvu kubwa kukushawishi ukiingia kwenye anga zao ujue muda wake umekwisha na utaishia kusugua benchi mpaka ukumbuke maisha ya kule ulikokuwa.

Sijakataza wachezaji kuondoka kwenye timu walizopo kwa sasa kwa kuwa maisha ya soka kwa sasa ni biashara ila muhimu kuangalia biashara unayoifanya ni ya muda gani na kwa manufaaa yapi?

Kama kuna ulazima wa kufanya biashara hiyo wakati huu basi ruksa ila kama utashauriwa hasa na benchi la ufundi wakakuambia muda wako bado waskilize kwani wao wanatambua vyema maisha ya soka la Bongo yalivyo hivyo unapaswa kuwa mtulivu usifanye papara

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic