MAMA mzazi
wa Luis Suarez aitwaye Sandra alikuwa ni mfagizi katika moja ya kituo cha
mabasi katika kitongoji cha Tres Cruzes Jiji la Montevideo nchini Uruguay na
hakuwahi kukata tamaa kuhusiana na mwanaye kwamba atakuja kuwa mtu mkubwa na
maarufu siku moja duniani.
Katika kitabu chake cha Luis Suarez, Crossing The
Line, Suarez ameelezea namna Sandra alivyokuwa akihangaika na watoto wengi
aliokuwa akiishi nao licha ya umasikini wake na kufanya asiwe na muda wa
kumuuliza kuhusiana na shule hasa maendeleo yake.
Pamoja na hivyo, ameeleza
namna mama yake alivyoendelea kumpa moyo na kumuasa kuendelea kupambana kwa
kile anachokiamini kwa kuwa hakupenda kumpangia. Baba yake mzazi, Rodolfo
Suarez alikuwa ni mwanajeshi, baadaye akaamua kuondoka jeshini na maisha
yakawa magumu zaidi hadi kufikia kuanza kujitafutia riziki kwa kufanya kazi
katika kiwanda cha biskuti na baadaye kuamua kujihusisha na ujenzi. Kuna
wakati Rodolfo hakuwa hata na fedha ya kujilipia kodi ya pango tu na
kulazimika kulala katika eneo walilokuwa wakifanya ujenzi ili kujisitiri.
Suarez anazungumzia namna umasikini ulivyowafanya wazazi wake washindwe
kwenda kumuunga mkono wakati akienda mazoezini katika klabu ya watoto ya
Nacional, moja ya klabu maarufu nchini Uruguay. Pamoja na hivyo, Suarez
ameeleza anavyoendelea kuwashukuru wazazi wake kwani licha ya kutomuunga
mkono kwa vitendo walikuwa wakimpa maneno ambayo yalimfanya aendelee
kupambana bila ya kuchoka na mwisho anamtaja mkewe Sofi Balbi kuwa ndiye
shujaa wake. Suarez na Sofi sasa wana watoto watatu, binti Delfina
(alizaliwa 2010) na wavulana wawili, Benjamin (alizaliwa 2013) na Lauti,
aliyezaliwa 2018. Walianza kuwa wapenzi Suarez akiwa na umri wa miaka 15 na
Sofi akiwa na 13.
Mshambuliaji huyo mtukutu sasa ana umri wa miaka 13 na
chanzo cha mafanikio yake ya mpira ni Sofi na ndiyo maana anamuona ni shujaa
wake lakini mji ulio katika historia ya maisha yake ni Barcelona.
Huenda
hapa inakuwa ni nafasi nzuri ya kujua kisa cha yeye kufikia kumwaga chozi
wakati anaondoka katika klabu hiyo na kwenda kujiunga na Atletico Madrid
ambao ni moja ya wapinzani wakubwa wa Barcelona kutoka katika Jiji la
Madrid. Baada ya kocha mpya wa Barcelona, Ronald Koeman kuonekana hana
mpango wa kumtumia au hana mpango naye, ikaelezwa atajiunga na Juventus ya
Italia na kuungana na Cristiano Ronaldo. Akiwa katika hatua za mwisho,
ikabainika kuwa alifanya udanganyifu wakati akitafuta uraia wa Italia ambao
anao. Hivyo ikawa ni kesi ambayo mwisho ilionekana anastahili kubaki nao
lakini kukawa na ugumu tena kujiunga na Juve. Ofa ya Atletico, mwisho
imefanikiwa kama mchezaji huru lakini mwisho aliangua kilio kama mtoto
akijua anaondoka Barcelona.
Wengi wanaweza kudhani ni mapenzi pekee na klabu
hiyo ambayo wana kauli mbiu yao “Zaidi ya Klabu”. Suarez lazima atakuwa
anakumbuka maisha ya Barcelona ambayo alijiunga nao mwaka 2014 akitokea
Liverpool na kufanikiwa kuichezea mechi 191 na kufunga mabao 147, hivyo
kuandika rekodi ya kuwa mmoja wa washambulizi hatari zaidi waliowahi
kuichezea Barcelona.
Lazima ndani ya Barcelona kuna umoja, ukaribu na
urafiki. Lakini aina ya mashabiki ambao Suarez atawakumbuka na mazoea kama
mwanadamu wa kawaida, hivyo ni lazima kumwaga chozi. Yote sawa, lakini kama
utabahatika kusoma kitabu chake hicho utagundua mapenzi yake na Barcelona
hayakuanza wakati anakwenda kujiunga nayo lakini Barcelona imo ndani ya
maisha yake kupitia Sofi.
Suarez hakupenda shule, ukizingatia familia yake
ilikuwa ni ya kimasikini sana, hawakuwa na muda wa kuifuatilia sana mienendo
yake shuleni. Lakini Sofi alipinga mara zote na kumhimiza kusoma. Muda
mwingi, Suarez alilazimika kuazima nauli asafiri zaidi ya kilomita 30 kwenda
kumtembelea Sofi nyumbani kwao. Baadaye familia ya Sofi ilihamia Ulaya,
ilihamia jijini Barcelona mwaka 2003 na huu ndio ulikuwa mwanzo wa Suarez
kutamani kwenda kucheza barani Ulaya kwa kuwa alitaka tena kuungana na Sofi
ambaye alimuona ndiye tegemeo katika kila kitu kwake. Mara moja, alialikwa
Ulaya na Sofi na bado anavyokumbuka walivyoibia kwenda kupiga picha ndani ya
Uwanja wa Camp Nou kwa kuwa hawakuwa na fedha za kulipia zoezi la kutembelea
uwanja huo. Unaona namna maisha yalivyokuwa na baada ya kurejea Uruguay,
aliamua kufanya juhudi kuu, akapambana hadi alipofanikiwa kusajiliwa na
klabu ndogo ya Groningen ya nchini Uholanzi, hii ilikuwa ni mwaka 2006.
Suarez aliongeza juhudi akijua alistahili maisha bora kwa kuwa Ulaya ni
mapambano zaidi na mara nyingi alitaka kumridhisha Sofi kwa kuwa alijua
alivyompigania na yeye hakuwa na elimu wala hakuwahi kufaulu, hivyo
alipambana akijua mkombozi ni mpira. Alifanikiwa kujiunga na Ajax mwaka
2007, mwaka 2011 akatua Liverpool na 2014 ikawa ni Barcelona lakini kumbuka
mwaka 2013 alitaka kujiunga na Arsenal lakini Steven Gerrard wakati huo
akiwa nahodha wa Liverpool, alimzuia na kumueleza acheze msimu mmoja akiwa
Anfield na huenda akajiunga na Real Madrid, Bayern Munich au FC Barcelona na
si Arsenal tena, na kweli msimu uliofuata, hilo likatokea.
Unaona kiasi gani
Mji wa Barcelona ulivyokuwa sehemu ya kumvuta Suarez kwenda Ulaya, kwa kuwa
ulikuwa mji wake wa kwanza kukanyaga akiwa Ulaya lakini mapenzi yake na
Barcelona, yalimfanya asichoke sababu alitamani siku moja ataichezea. Bila
shaka ilikuwa ni klabu yake pendwa ambayo alifanikiwa kuifikia. Sofi,
anabaki kuwa shujaa wake kwa kuwa unaona alivyoshiriki katika maisha yake
wakiwa watoto kutoka katika familia zenye aina tofauti kabisa. Kwani baba
mzazi wa Sofi alikuwa bosi wa benki na walihama baada ya benki kufungwa
kutokana na anguko la kiuchumi mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Chozi la Suarez
si kuondoka tu FC Barcelona, linajumuisha mengi na “undugu” wa historia ya
maisha yake na Jiji la Barcelona, unamfanya akumbuke mengi aliyopitia akijua
sasa anahamia katika jiji pinzani la jiji lake kipenzi, timu yake kipenzi
lakini maisha, hayakupi nafasi ya kuchagua kila unachokitaka kama leo Suarez
ni tajiri, maisha yake ni ya kifahari kwa kuwa mshahara wake kwa mwaka
utakuwa zaidi ya pauni milioni 6 (zaidi ya Sh bilioni 17), lakini hana
ujanja, lazima aondoke Barcelona kwa maana ya klabu na jiji pia.
0 COMMENTS:
Post a Comment