ARISTICA Cioaba, Kocha Mkuu wa Azam FC, amewaambia mabosi wake kuwa anahitaji mechi moja ya mwisho kwa ajili ya kulipima jeshi lake kabla ya kuanza mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo ametaka mechi hiyo ikiwa ni ya mwisho kwa ajili ya kutesti mitambo yake mipya ambayo imesajiliwa kwa msimu huu kabla ya kuanza kusaka pointi kwenye ligi.
Azam FC imeshacheza mechi tatu za kirafiki zikiwemo dhidi ya Namungo FC katika Azam Festival ambapo ilishinda 2-1, KMC waliyoshinda bao 1-0 na Prisons walitoka sare ya kufungana bao 1-1.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ ameliambia Championi Jumatano, kuwa mechi hiyo imetakiwa na kocha wao huyo raia wa Romania kwa ajili ya kujiweka sawa kabla ya mechi yao ya kwanza ya ligi.
“Bado kocha ametaka mechi moja ya kuangalia wachezaji wake.Baada ya hapo tutakuwa tayari kuanza kushiriki ligi ya msimu huu, ila kwa asilimia kubwa tuko tayari kwa ajili ya kuanza na kutoa ushindani kwenye mechi zetu za ligi.
"Hatuna mashaka ikiwa tutashindwa kuipata mechi hiyo ila tupo tayari kwa ajili ya kuanza kupambana kwa msimu mpya wa 2020/21," aliweka nukta Popa.
Azam FC itamenyana na Polisi Tanzania, Septemba 7, Uwanja wa Azam Complex kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 6.
0 COMMENTS:
Post a Comment