BEKI wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Klabu ya Mtibwa Sugar, Dickson Job, amesema kuwa nahodha wa Stars, Mbwana Samatta hapaswi kulaumiwa kutokana na matokeo ya kupoteza kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Burundi.
Stars ilipoteza kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa uliochezwa Oktoba 11 na Mbwana hakuyeyusha dakika zote 90 kutokana na kutolewa kwa kuwa alionyeshwa kadi moja ya njano.
Kiungo Jonas Mkude yeye alionyeshwa kadi mbili za njano na kusababishwa aonyeshwe kadi nyekundu dakika ya 77 na Martin Saanya.
Job amesema: “Tumepoteza mchezo uliopita dhidi ya Burundi lakini cha kushangaza ni kwamba watu wengi wamekuwa wakimlaumu nahodha wetu, Mbwana Samatta, lakini kwa upande wangu naamini tulipoteza mchezo kutokana na makosa ya pamoja.
“Naamini benchi la ufundi likiongozwa na kocha Ndayiragije limeyaona na litahakikisha yanafanyiwa kazi kabla ya safari yetu ya kwenda Tunisia kwa ajili ya mchezo wetu wa Novemba 13 dhidi ya timu ya Taifa ya Tunisia, katika jitihada za kuhakikisha tunafuzu michuano ya AFCON 2021,” amesema Job.
0 COMMENTS:
Post a Comment