JUMA Mwambusi, Kocha Msaidizi wa Yanga amesema kuwa wachezaji wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Uwanja wa Mkapa majira ya saa 1:00 usiku.
Yanga inaingia uwanjani ikiwa imetoka kupata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro pia ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM ya Zanzibar na ilishinda mabao 2-0.
Akizungumza na Saleh Jembe, Mwambusi amesema kuwa maandalizi ambayo wanayafanya yanawapa imani ya kupata matokeo kwenye mechi ambazo wanazicheza jambo ambalo linawapa hali ya kujiamini.
"Ukiwa na kikosi chenye uhitaji wa matokeo inakuwa ni rahisi kuamini kwamba utapata matokeo hivyo tutawafuata wapinzani wetu kwa kuwaheshimu ila tunahitaji pointi tatu.
"Mechi zetu za hivi karibuni zimekuwa zikitupa picha ya kile ambacho tunakikosea ila sio tatizo kushinda kwa bao moja kwenye mechi ambazo zimepita kwani ni wakati wetu wa kuangalia namna gani tunaweza kushinda zaidi.
"Uwepo wa wachezaji wengi wageni ni sababu pia hata ukiangalia kwamba kwenye muda wa kuanza mazoezi hatukuwa na muda mrefu tunachokifanya ni kutengeneza muunganiko ambao utakuwa imara kwetu," amesema.
Coastal Union imeshinda mchezo mmoja mbele ya JKT Tanzania kwa kupata bao 1-0 huku ikipoteza mechi mbili na kulazimisha sare moja mbele ya Dodoma Jiji FC.
Yanga wao wameshinda mechi tatu na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 mbele ya Tanzania Prisons hivyo mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Msimu wa 2019/20 walipokutana uwanjani, mchezo wa kwanza Yanga ilishinda kwa bao 1-0 Uwanja wa Uhuru na mchezo wa pili uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga walitoshana nguvu na kugawana pointi mojamoja.
0 COMMENTS:
Post a Comment