ABDULHAMN Mussa, nyota wa Klabu ya Ruvu Shooting leo amekuwa shujaa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara Uwanja wa Uhuru wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 baada ya kuichezesha pira gwaride Mbeya City.
Mussa alianza dakika ya 11 kutoa pasi ya bao kwa Wlliam Patrick aliyefunga bao la kuongoza. Bao hilo lilidumu mpaka muda wa mapumziko.
Kipindi cha pili Mbeya City ilianza kwa kuchangamka kidogo kwa kufanya majaribio ya kuweka usawa ngoma ilikuwa nzito na dakika ya 53 ilikutana na balaa la guu la Mussa aliyepiga mpira wa adhabu nje ya 18 ukazama langoni na kumuacha mlinda mlango wa Mbeya City akiwa hana chaguo.
Dakika ya 90 zikiwa zikiwa zimeongezwa dakika tatu mpira kukamilika, Mussa tena alimtengenezea pasi Fully Maganga aliyepachika bao la tatu kwa Ruvu na kuwafanya wasepe na pointi tatu mazima.
Charles Mkwasa, Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting amesema kuwa wachezaji wake walipambana kupata pointi tatu jambo ambalo wamefanikiwa.
Ushindi huu unaifanya Ruvu Shooting kuwa ya moto ndani ya Uwanja wa Uhuru kwa kuwa kwenye mechi zake za hivi karibuni imekuwa ikisepa na pointi tatu.
Iliawatungua Simba bao 1-0 ikiwa ugenini Uwanja wa Uhuru na iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Coastal Union na leo imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City.
Kwenye mechi zake tatu za hivi karibuni imeshinda zote na kufunga mabao saba huku wao wakifungwa bao moja pekee.
Ushindi huu unaifanya ifikishe jumla ya pointi 19 na kuishusha Biashara United nafasi ya nne kwa kuwa leo imelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji na kuifanya ifikishe pointi 18.
Mbeya City bado hali sio shwari ikiwa imesalia nafasi ya 17 na pointi zake saba baada ya kucheza mechi 11.
0 COMMENTS:
Post a Comment