KUHUSU ubingwa wa Kombe la Mapinduzi tayari kwa sasa wale ambao waliotwaa wameanza kusahau yale machungu ambayo walikuwa wanapitia katika kuusaka.
Ipo wazi kwamba Yanga ni mabingwa wapya ambao waliweza kutwaa taji hilo baada ya kushinda mbele ya watani zao wa jadi, Simba wanastahili pongezi kwa hilo ambalo wamelifanya.
Tumeona kwamba Mtibwa Sugar bado haijwa imara kwenye ushindani kutokana na kushindwa kuendeleza makali yake ndani ya uwanja na kushuhudia taji hilo likiondoka mikononi mwao.
Upande wa wenyeji ambao ni Chipukizi, Jamhuri,Malindi,Mlandege hawa hawakuwa na wakati mzuri ni muhimu kujipanga kwa ajili ya wakati ujao ili kuwa imara zaidi na kupata matokeo mazuri.
Kwa muda mrefu, wenyeji hawajawa na mwendo mzuri katika kupata matokeo ndani ya uwanja hivyo ni muhimu kujikumbusha kwamba nyakati zijazo ni muhimu kwao kuweza kupambana kupata matokeo mazuri.
Kwa waandaaji nina amini kwamba changamoto ambazo wamezipata mwaka huu nazo ni lazima kufanyiwa kazi ili mwaka ujao iwe na ushindani mkubwa mara dufu.
Kwa sasa mambo mengi yamebadalika na mipango pia inabidi ibadilike ili kwenda sawa na ushindani uliopo kwenye uwanja wa mpira kiujumla bila kumuacha hata mmoja nyuma.
Nasema hivyo kwa sababu miaka ya nyuma ushindani ulikuwa ni mkubwa na timu nyingi ambazo zilikuwa zinashiriki zilikuwa zinanguvu kubwa hali ambayo ilikuwa ni ngumu kuweza kumtambua mshindi.
Kila mmoja alikuwa anapiga hesabu za kuwa bingwa hali ambayo ilifanya kila mchezo kuwa na msisimko wa kipekee.
Miaka ya hivi karibuni wamekuwa wenyeji pekee wanashiriki Kombe la Mapinduzi na wageni ambao ni wamoja hawa kutoka Bara hivyo ninaona kwamba ni muhimu kuweza kuboresha pia kwa timu shiriki kurejesha ushindani.
Nadhani kwamba janga la Corona mwaka jana linaweza kuwa sababu kwa timu nyingine kushindwa kuja kushiriki ila wakati ujao itapendeza ikiwa zitaongezeka na nyingine kutoka nje ya nchi.
Mashindano haya yamekuwa na matokeo mazuri kwa baadhi ya wachezaji ambao walikuwa hawapati nafasi kikosi cha kwanza kwa kuwa wameweza kuonekana na kufanya kazi nzuri ndani ya uwanja.
Pia ni wakati wa kutazama na masuala ya ratiba namna inavyoweza kuwa rafiki pamoja na kubadili mfumo hasa wa uendeshaji isiwe ni bonanza ambalo linashirikisha timu kubwa na ndogo bali iwe kwenye mfumo wa ligi.
Ikiwa itakuwa kwenye mfumo wa ligi itafanya mashabiki wapate ladha nzuri zaidi huku timu zikipata muda wa kufanya vizuri ndani ya uwanja kwa kuwa mechi zao zitakuwa na muda maalumu ambao utapangwa.
Kwa wakati huu tumeona namna Namungo ambayo imeshiriki Kombe la Mapinduzi kwa mara ya kwanza na imeweza kuonyesha ushindani.
Katika hilo wanastahili pongezi kubwa na wakati ujao wazidi kuongeza juhudi ili kufanya vizuri zaidi. Wakati wa kupeperusha bendera na kuongeza ubora katika mashindano yetu ya ndani ni sasa.
Somo jipya kwa waandaaji ni kwamba wanapaswa waangalie namna mpya itakayowasaidia waweze kuibuka na mvuto mpya hasa kwa kuanzia na maboresho ya ratiba.
Wakifanikwa kucheza na ratiba itawafanya wawe na uwanda mpana kwa washiriki kuwa huru kucheza kwa ushindani bila kuwa na hofu yoyote kitaifa na kimataifa.
Ukiweka kando suala la Kombe la Mapinduzi kwa sasa timu yetu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ipo Cameroon ambapo inashiriki mashindano ya wachezaji wa ndani, (Chan).
Jambo la msingi kwa wachezaji ni kuongeza juhudi na kufanya kazi kwa moyo katika kusaka matokeo ndani ya uwanja ili kupeperusha vema bendera ya Tanzania.
Hakuna Mtanzania ambaye anapenda kuona timu inayumba na kupata matokeo mabovu kimataifa kila mmoja anapenda kuona timu ikipata matokeo mazuri ndani ya uwanja.
Hatua ambayo tupo kwa sasa sio ya kuibeza inahitaji umakini na kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa wakati kwa kuwa kazi ya mchezaji ni kusaka ushindi ndani ya uwanja.
Pia kumekuwa na suala la usajili ambao umefungwa hivi karibuni hivyo ni wakati wa wachezaji kuonyesha kile ambacho kimewavutia mabosi wao ndani ya timu mpya.
Wale ambao wamesajili wakati wao sasa kuonyesha yale ambayo wanatakiwa kuonyesha ndani ya uwanja kwa kupambania timu zao zifikie malengo yao.
Pia Ligi ya Wanawake nayo pia imekuwa ikendelea na ushindani huku ni mkubwa kwa kila timu kuwa na nia ya kufanya vizuri ndani ya uwanja.
Kwa zile ambazo zilikuwa zinakwama kupata matokeo ndani ya mechi zao ambazo wamecheza ni wakati wao wa kujipanga upya na kuanza kwa namna nyingine.
Ni muda wa kumaliza hesabu kwa kuwa mzunguko wa pili ushindani wake huwa unakuwa tofauti zaidi ya mzunguko wa kwanza.
Hesabu ambazo zimekwama kukamilika mzunguko wa kwanza inapaswa zimaliziwe mzunguko huu wa pili ambao huwa unakuwa na ushindani mwanzo mwisho.
Wakati huu mbivu na mbichi zitajulikana kwa zile ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja na kwa zile ambazo zinawania taji la Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili ni muda wa mavuno.
0 COMMENTS:
Post a Comment