WAKATI wa Watanzania kuendelea kuipa sapoti timu ya Taifa ya Tanzania ambayo inawakilisha nchi kwenye mashindano yanayoshirikisha wachezaji wa ndani, Chan ni sasa.
Matokeo ambayo yametokea januari 19 kwa Stars kupoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia yatabaki kuwa somo kwa wachezaji na wanachotakiwa kukifanya ni kuongeza zaidi juhudi katika kusaka ushindi ndani ya uwanja.
Imani yangu ni kwamba kila Mtanzania anapenda kuona timu ya Tanzania inafanya vizuri.Ni mwendelezo mzuri wa kuipa sapoti timu katika kila namna ili kuweza kupeperusha bendera kimataifa.
Kwa wakati huu wachezaji ni muhimu kuongeza juhudi ndani ya uwanja ili kuweza kufungua ukurasa wa kupata timu nyingine nje ya nchi na inawezekana ikiwa kutakuwa na juhudi isiyo ya kawaida.
Nina amini kwamba wakati huu wa haya mashindano ya Chan wapo ambao watafungua ukurasa wao mpya wa kutoka katika ulimwengu wa mpira. Njia ni moja tu kwa wachezaji kucheza kwa juhudi na kusaka matokeo bila kukata tamaa.
Mapambano ni lazima kuendelea siku zote bila kurudi nyuma kwa kuwa kwa sasa hakuna muda wa kurudi nyuma jambo la msingi ni kusonga mbele kusaka ushindi na kufanya vizuri zaidi ya jana.
Huu ni mwaka mpya wa 2021 yale mambo ambayo yalifanyika mwaka uliopita ni lazima yawekwe kando na kwa sasa iwe ni muda wa vitendo zaidi ndani ya uwanja pamoja na kufanya mambo ambayo yatakuwa ni furaha kwa mashabiki pamoja na taifa kiujumla.
Tofauti ambazo zilikuwepo nyuma kwa mashabiki kugawana makundi kila mmoja kuwa na kundi lake kwa sasa hilo halipaswi kupewa kipaumbele zaidi ni kwamba kila mmoja anapaswa kuipa sapoti Stars.
Ukiachana na hayo sasa twende kwenye mada ya leo ambapo ningependa kuzungumzia kuhusu Ligi ya Wanawake Tanzania.
Miaka ya nyuma ligi hii ilikuwa haina umaarufu na wala ilikuwa haifuatiliwi kwa ukaribu. Ila kwa wakati huu kumekuwa na mabadiliko makubwa ambapo wengi wanafuatilia hii ligi.
Msimu huu wa 2020/21 kumekuwa na ushindani wa kipekee huku kwenye Ligi ya Wanawake ambapo kila timu inaonekana kujipanga kufanya vizuri.
Ipo wazi kwamba kila timu kwa sasa imejipanga vizuri kupata matokeo. Licha ya kwamba zipo timu ambazo zimekuwa na matatizo ya masuala ya uendeshaji hasa kwenye suala la uchumi.
Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) wanapaswa wajipange sawasawa kulidhibiti hili kwani kwa kuanza kuvurunda mwanzo kutafanya ule msisimko ambao umeanza kuishia njiani.
Jambo lingine pia la kuzingatia ni ubora wa viwanja ambavyo vitakuwa vinatumika katika kusaka matokeo ndani ya uwanja.
Timu zote 12 zinazoshiriki Ligi zina nafasi ya kufanya vizuri ikiwa zitazingatia maandalizi mazuri kila kitu ni maandalizi na wakati wa kufanya maandalizi ni sasa kupitia makosa ambayo yanafanyika.
Benchi la ufundi pamoja na viongozi wanapaswa waangalie kwa umakini ni wapi walipokosea 2020 ili wafanikiwe kusonga mbele na kupata matokeo katika michezo yao ijayo.
Kikubwa ambacho wachezaji wanapaswa wakifanye ni kujitambua na kubeba nguvu ya kujiamini kwamba wanaweza kupata matokeo uwanjani kwa kupambana bila kuchoka.
Jambo la msingi kwa sasa ni kila timu kupambana ndani ya uwanja kusaka matokeo chanya kwani kila timu ndani ya uwanja inahitaji ushindi hakuna inayofikiria kuhusu kupoteza.
Imani yangu ni kwamba ushindani ukiwa mkubwa huku kwa Wanawake itaongeza nguvu ya kuwa na timu ya Taifa ya Tanzania yenye nguvu.
Kama wachezaji mtaamua kujituma uwanjani pasipo kumtegemea mchezaji mmoja maana yake ni kwamba mtapata matokeo mazuri ambayo mnayafikiria.
Ila kama kila mmoja atakuwa anajiona yeye ni bora kuliko mwingine hapo ndipo tatizo linapoanzia hasa kwa kufanya ushindani na ule ubora kupotea.
Uongozi wa timu zote kwa sasa una jukumu la kutazama wapi ambapo walikuwa wanakwama kupata matokeo kwenye mechi zao zilizopita.
Kila mmoja akubali kujitoa kwa ajili ya timu na afanye kazi kwa juhudi akiwa uwanjani bila kujali anacheza na nani uwanjani.
Tunaamini kwamba tunaweza kufanya mapinduzi katika soka la Wanawake na kuipeperusha bendera ya taifa nje ya nchi.
Ushindani ni mkubwa kwa sasa ndani ya uwanja hivyo ni fursa kwa wachezaji kuogeza juhudi ndani ya uwanja katika kila mechi ambazo watakuwa wanacheza.
Hivyo ni muhimu wachezaji wetu pia kuweka kwenye akili kwamba wapo sokoni wanapoingia ndani ya uwanja na wanaweza kufikia mafanikio na kucheza nje ya Bongo.
Wengi wameanza kufuatilia ligi ya Wanawake Tanzania hili ni jambo jema hivyo basi sapoti inahitajika ili kuwa imara zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment