Na Saleh Ally
NANI aliye nyuma ya wanaotaka
kuandamana eti kwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela
amefungiwa miaka mitano baada ya kupatikana na hatia ya kuzungumza maneno ya
uchochezi.
Kamati na Maadili ya Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) ilitangaza kumfungia Mwakalebela kwa miaka mitano na faini
ya jumla ya Sh milioni tano kutokana na makosa mawili.
Kwanza ni uchochezi kwa mashabiki wa
Klabu ya Yanga dhidi ya vyombo vinavyosimamia akidai vinaihujumu Yanga,
alivyoitwa katika kamati hiyo ya maadili alishindwa kuthibitisha.
Kosa la pili ni kusema alikuwa na
mkataba baina ya Bernard Morrison na Simba na aliuonyesha mbele ya waandishi wa
habari lakini Kamati ya Maadili imeeleza kwamba alishindwa kuuonyesha kwao
mkataba huo na kuthibitisha kile alichokizungumza mbele ya waandishi wa habari.
Adhabu alizopewa Mwakalebela
zimeelezwa kwa mujibu wa vifungu vya 73 (4) cha Kanuni ya Maadili na 6 (1)
(b) na 6 (1) (c) cha Kanuni ya Maadili pia.
Wakati Mwakalebela akiwa ameanza
kutumikia adhabu hiyo, kumeibuka hoja kadha wa kadha kuhusiana na adhabu hiyo
na wako wamekuwa wakiishambulia TFF katika hili.
Inawezekana ni kutuelewa mambo na
hili limekuwa likiendelea kwa kuwa TFF ina kamati ambazo ni huru na zina uwezo
hata wa kumfungia kiongozi wa shirikisho hilo. Wanaoamua si wafanyakazi wa TFF
badala yake wadau mbalimbali wanaokuwa wameteuliwa kuendesha kamati hizo.
Mwakalebela angeweza kuthibitisha
alihojiwa maana yake kusingekuwa na udhia huo. Kilichotokea imeonekana hana huo
mkataba wa Morrison kama alivyosema na kashindwa kuthibitisha kwamba TFF na
Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), zinaihujumu Yanga na adhabu ikafuatia.
Nianze na kusema bila ya ubishi, kama
ilivyoeleza kamati ya maadili, kama Mwakalebela alishindwa kuthibitisha
aliyoyasema, anastahili adhabu kabisa.
Lazima kuwe na weledi katika
uzungumzaji, viongozi wapunguze mihemko katika mambo ya msingi na wanapaswa
kuwa na staha kuepusha kusababisha athari na chuki ndani ya mchezo wa soka.
Viongozi wengi hasa wa klabu hizi
kubwa, wana tabia wanakosea halafu baada ya hapo wanatafuta kisingizio kwa
kuwaangushia mpira TFF au wadau wengine na silaha yao imekuwa mashabiki, hili
limekuwa kawaida.
Pili, pamoja na kuwaadhibu, bado
ninasisitiza kwamba adhabu ziwe zile ambazo zinawafanya watu wajifunze na
kurejea kufanya yaliyo sahihi. Adhabu ya miaka mitano inakuwa ni sawa na
kumfungia mtu kifungo cha maisha. Miaka mitano ni mingi sana na adhabu inakuwa
ni kama ya kukomoana.
Hata adhabu ya fedha, nayo ni kubwa
sana. Bado inawezekana ikawa chini ya hapo na bado ikawa fundisho kwa mhusika
lakini isiwe kama ndiyo itakuwa adhabu ya mwisho kutolewa. Hivyo kuna kila
sababu ya kuzipitia hizo kanuni mbili na nyingine za Kamati ya Maadili maana
zinakuwa zinaumiza na kukomoa badala ya kuumiza na kubadilisha.
Mwisho ni mashabiki hasa wale baadhi
ambao wameingia na mihemko bila ya kuingia ndani ya mistari ya usahihi
kuangalia kipi sahihi ambacho kinaweza kufanyika.
Kuandamana ili iweje? Mwakalebela
kashindwa kuthibitisha kwenye kamati, kuandamama ili iweje wakati Mwakalebela
kapatikana na hatia. Acheni hoja dhaifu eti alizungumza kwa niaba ya klabu,
sote tunajua kanuni inambana muhusika au aliyezungumza bila ya kujali ni kwa
niaba ya klabu au yeye mwenyewe na washkaji zake.
Hivyo kuwe na namna ya kuheshimu
mamlaka na kuepuka kujiona wakubwa sana wakati sivyo. Ukishakuwa na kundi lako,
basi unaona hakuna kama nyie na mnaweza kusema lolote, si sahihi hata kidogo.
Nyongeza, si kila jambo likiwatokea
Yanga lazima wafananishe na Simba au ikumbushiwe Simba. Alichokosea,
alichoadhibiwa vinaweza kuwa mjadala bora ambao ukatoa funzo badala ya kuingiza
yasiyohusika.
Adhabu hizi ni msumeno, zinakata huku
na kule. Lakini lazima tukubali kuzipitia na mwisho kufikia ule mwafaka
unaokuwa ni kuadhibu kwa ajili ya kurekebisha na kutengeneza ubora sahihi.
0 COMMENTS:
Post a Comment