RENATUS Shija, Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji amesema kuwa kesho watawashangaza wapinzani wao Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Mkapa.
Dodoma Jiji ambayo kwenye msimamo ipo nafasi ya 6 na pointi zake 38 inakutana na Simba iliyo nafasi ya kwanza na pointi zake ni 58.
Mchezo wa kwanza walipokutana Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ubao ulisoma Dodoma Jiji 1-2 Simba baada ya dakika 90 jambo lililowafanya Dodoma Jiji kuyeyusha pointi tatu mazima.
Akizungumza na Saleh Jembe, Shija amesema kuwa wamejipanga kwa ajili ya mchezo wa kesho kimbinu na wanaamini kwamba watawashangaza wapinzani wao.
"Kesho tutawashangaza wapinzani wetu uwanjani kwa kuwa mipango yetu ipo sawa na mbinu imara hasa kuona kwamba tunapata pointi tatu muhimu.
"Tunatambua kwamba mchezo utakuwa mgumu ila kwa maandalizi na utayari wa wachezaji tunaamini kwamba tutapata ushindi mbele ya Simba.
"Ubora wa wapinzani wetu tunajua upo wazi ila nina amini kwamba watakuwa bora zaidi ikiwa sisi tutakuwa dhaifu hivyo ni muhimu kwetu kupambana na kusaka ushindi hilo linawezekana, mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti," amesema.
Dodoma Jiji ilitia timu Dar jana Aprili 25 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya mwisho na leo pia imefanya mazoezi kwa ajili ya mchezo huo Uwanja wa Mkapa.
Itakuwa ni saa 1:00 usiku na ikumbukwe kwamba ule wa kwanza, Dodoma ulichezwa saa 10:00 jioni.
Maneno hayo, waulize mtibwa
ReplyDelete