KUELEKEA katika mchezo wao wa kesho Jumamosi dhidi ya Yanga, Uongozi wa kikosi cha klabu ya KMC umeichimba mkwara mzito Yanga kwa kuweka wazi kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo.
Yanga na KMC kesho zitashuka kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa mwendelezo wa Ligi Kuu Bara iliyorejea rasmi jana Alhamisi, baada ya kuwa kwenye mapumziko ya siku 21 za maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk John Pombe Magufuli.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza kati ya timu hizo uliopigwa Oktoba 25, mwaka jana katika uwanja wa CCM Kirumba uliisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Akizungumzia maandalizi yao kocha msaidizi wa KMC, Habibu Kondo alisema: “Tumekuwa na maandalizi mazuri ya kikosi chetu kuelekea michezo yetu ijao ya kombe la Shirikisho pamoja na Ligi Kuu Bara hususani mchezo wetu ujao dhidi ya Yanga.
“Tunajua mchezo huu utakuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wetu lakini hatuna hofu kwani tunafanya maandalizi ya kutosha, na tuna imani kubwa ya kupata matokeo mazuri dhidi yao ili kutimiza malengo yetu,”
KMC wanakamatia nafasi ya tano
kwenye msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 35 kwenye michezo 24
waliyocheza mpaka sasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment