April 9, 2021


NIMEWASIKIA baadhi ya viongozi wanaowasimamia waamuzi wanaochezesha Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la kwanza wakijaribu kuwaasa kuwa makini kwakuwa tunakwenda katika kipindi maarufu sana cha lalasalama.

 

Kipindi hiki kinakuwa na uamuzi wa mambo mbalimbali ambayo yanakuwa ni yakufurahisha na kuumiza kwa timu za soka ambazo zinashiriki iwe ni ligi kuu au ligi daraja la kwanza.

 

Ukiwasikiliza viongozi hao, wamesema kwamba wanajua kwamba ligi inakwenda ukingoni na kunakuwa na mambo mengi,hivyo waamuzi wanapaswa kuwa makini kutokana na hali hiyo.

 

Hatuwezi kusema waamuzi wa ligi kuu au daraja la kwanza ni wageni na ligi hizo na kama wapo, basi ni wachache  lakini watakuwa   wanajua mengi kuhusiana na ligi hizo.

 

Kipindi cha lala salama kweli kina mambo mengi kwa kuwa ndio wakati kila timu itakuwa inapambana kutetea uhai wake au ndoto zake ambazo zilikuwa zinatakiwa kutimizwa wakati wa kipindi hicho cha lala salama.

 

Walio juu watakuwa wanauhakika wa kubaki, wanachotaka ni ubingwa. Walio katikati wanataka kuongeza pointi kujihakikishia kubaki katika ligi na waliomkiani maishani hofu kila mmoja anataka kujikomboa.

 

Bahati nzuri ligi yenyewe kupitia ratiba yake inakuwa haichagui wa kwenye nafasi ya ngapi atakutana na aliye katika nafasi ipi. 

Ndio maana utaona anayewania ubingwa anakutana na aliyemkiani, anayewania kubaki anakutana na anayewania ubingwa.

 

Ugumu wa ligi unaongezeka kwa kuwa kila timu haikubali kufungwa na utaona namna kunavyokuwa na ugumu kwa kuwa kila mmoja anakuwa anazipambania pointi. Kuliko kukosa zote, angalau hata kupata pointi moja hivi.

 

Aina ya uchezaji inabadilika, juhudi zinaongezeka na kila timu inakuwa inaona kufungwa ni kama dhambi kubwa hata kama ilipoteza mechi 15 katika 20 ilizocheza.

 

Kipindi hiki ndicho utasikia timu iliyomkiani imeshinda  dhidi ya mabingwa watetezi au vinara wa ligi hiyo. Hii inatokana na timu hiyo kuwekeza nguvu nyingi katika suala la kubaki katika ligi.

Waamuzi, wanakuwa sehemu kubwa ya kufanya mambo yaende kwa usalama na uhakika na mwisho kama ni suala la ushindani basi liwe la uwanjani.

 

Unaona mara nyingi kumekuwa na shutuma kuhusiana na waamuzi na ukweli ni kwamba hizi  zinakwenda katika mambo mawili tu. Kwanza ni uhalisia, hofu ya kupoteza na wakati mwingine timu inakuwa haijajiandaavizuri, ikipoteza bila ya kuangalia upungufu wake, linafuatia suala la kwamba tumehujumiwa.

 

 

Pili ni suala la waamuzi kuonekana wanakosea sana katika kipindi hiki, jambo ambalo linawafanya wahusishwe na masuala ya rushwa, jambo ambalo wamekuwa wakilikanusha kwa juhudi kubwa sana.

 

 

Wanakataa na kukanusha, wako sahihi kwa kuwa rushwa ni mambo ya siri lakini kwa walio karibu na mpira wanajua kuna sehemu zinakuwa na walakini na kipindi hiki cha lala salama, kumekuwa na masuala haya mengi na hata malalamiko ni mengi.

 

 

 

Waamuzi wamekuwa wakihusishwa na rushwa au kukubali kuzipendelea baadhi ya timu ili ziweze kufanya vizuri na kufikia malengo yao na nyingi ni zile zinazoaminika kuwa zimetoa “mpunga”.

 

 

 

Hatuwezi kulibeza hili kwa kuwa sigeni na limekuwa likitokea mara nyingi sanasana na hasa katika kipindi hiki cha lala salama na vizuri ni kuwa kumbusha watukuwa wawe makini na suala la kuwa fair ndio lichukue nafasi.

 

Weledi uwe kiongozi wakati huu ili kuyafanya mambo yaende kwa usahihi, ushindani uwe sahihi na mwisho tupate bingwa na wengine walioshika nafasi fulani kwa uwezo wao kwa kuwa ha kiimetendeka.

 

Kama waamuzi watakuwa wanakubali kuchukua rushwa, basi wao ndio wanakuwa maadui wakubwa wa maendeleo ya mpira wa Tanzania.

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic