IMEELEZWA kuwa nyota watatu wa Klabu ya Simba wamewekwa kwenye rada za vigogo wa Afrika ambao wanahitaji kupata saini zao kutokana na uwezo ambao wameonyesha kwenye mechi za kimataifa pamoja na Ligi Kuu Bara.
Wa kwanza ambaye anatajwa kwa ukaribu kuweza kuwa kwenye rada za vigogo wa Afrika Kusini pamoja na Sudan ni kipa namba moja Aishi Manula ambaye yeye kwenye hatua ya makundi amecheza mechi tano, akifungwa mbili na mechi tatu hajaruhusu bao.
Huyu anatajwa kuwekwa kwenye rada za Al Merrikh ya Sudan na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo inahitaji kuipata saini yake kwa dau nono.
Pia mwingine ni Luis Miquissone, kiungo mshambuliaji ambaye amekuwa gumzo Afrika kutokana na uwezo wake akiwa ndani ya uwanja kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Bao lake alilowatungua Al Ahly, Uwanja wa Mkapa bado lipo kwenye kumbukumbu ya Caf kwa kuwa lilipewa tuzo ya kuwa bao bora la wiki.
Pitso Mosimane, Kocha Mkuu wa Al Ahly inaelezwa kuwa anahitaji kupata huduma ya mchezaji huyo ambaye aliwahi kufanya naye kazi miaka ya nyuma.
Nyota wa tatu ni Mwamba wa Lusaka ambaye utaratibu wake akiwa uwanjani umekuwa ukiwakasirisha mashabiki wengi licha ya kwamba ni mtindo wake ambao anautumia kila siku.
Chama anatajwa kuwa kwenye rada pia za timu kutoka Misri ambayo haijawekwa wazi.
Kuhusu wachezaji wa Simba kuhitajika kusepa, Kocha Mkuu Didier Gomes alisema kuwa kwa wakati huu hajafikiria kumuacha mchezaji muhimu kwa kuwa bado wana kazi ya kufanya kimataifa.
Simba imetinga hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni namba moja kwenye kundi A ina pointi 13 inafuatiwa na Al Ahly iliyo nafasi ya pili na pointi 11.
0 COMMENTS:
Post a Comment