RAPA wa Marekani, Earl Simmons maarufu kama DMX amefariki dunia Aprili 9, 2021 jijini New York akiwa na umri wa miaka 50.
“Tunasikitika kutangaza kuwa leo,(Jana) mpendwa wetu DMX, kwa jina la kuzaliwa Earl Simmons amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 50 katika Hospitali ya White Plains, familia yake ikiwa pembeni yake baada ya kuwekwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua kwa siku kadhaa,” taarifa ya familia imeeleza.
Rapa huyo alikuwa amelazwa hospitalini tangu wiki iliyopita baada ya kushambuliwa na mshtuko wa moyo akiwa nyumbani kwake jijini New York, kwa mujibu wa mwanasheria wake wa muda mrefu, Murray Richman.
Imeelezwa kuwa rapa huyo alizidisha matumizi ya dawa za kulevya.
DMX (Dark Man X) alianza kufanya muziki wa rap mwanzoni mwa miaka ya 1990. Mwaka 1998 alifanikiwa kuachia albam ya kwanza iliyoitwa ‘It’s Dar and Hell Is Hot.” Albam hiyo iliuza nakala 251,000 katika wiki ya kwanza tu.
Baada ya kifo cha nguli wa rapa Notorious B.I.G na Tupac Shakur, DMX aliibuka kuwa rapa anayetamba kwa nguvu kubwa zaidi na kuwa msanii wa kwanza kusaini mkataba wa kuwa mwanafamilia wa lebo ya Ruffhouse. Ngoma yake ya ‘Ruff Ryders Anthem’ ilimpa mafanikio zaidi na kuifanya dunia impokee kwa nguvu zaidi.
DMX aliachia albam kadhaa kwa miaka hiyo, lakini mwaka 1999 aliachia ‘And Then There Was X’ ikiwa ni moja kati ya albam zilizompa mafanikio zaidi kibiashara. Albam hiyo ilitajwa kuwania Tuzo za Grammy katika kipengele cha Albam Bora ya Mwaka.
Alifanikiwa kuuza albam zake kwa mamilioni ya nakala. Ngoma zilizompa nafasi zaidi ya kufanikisha hilo ni pamoja na ‘Get At Me Dog’ ya mwaka 1998, ‘Party Up,’ ya mwaka 1999’ na ‘X Gon’ Give It to Ya, ya mwaka 2003.
Mbali na muziki, DMX alijihusisha pia na filamu akiigiza katika filamu kadhaa. Filamu zilizopata umaarufu ni ‘Romeo Must Die’ na ‘Cradle 2 The Grave’ zote akiwa na Jet Li. Nyingine ni pamoja na ‘Exit Wounds’ na ‘Never Die Alone’.
Rapa huyo ambaye alishaingia kwenye matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya na kujikuta akitupwa jela kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kukiuka sheria, ameacha watoto wanne.
Apumzike kwa amani.
0 COMMENTS:
Post a Comment