April 13, 2021

 

BAADA ya kukamilisha ratiba ya michezo yao ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Uongozi wa kikosi cha klabu ya Simba umesema sasa nguvu zao zote wanaziwekeza katika michuano ya Ligi Kuu Bara, na kujinasibu kuwa wamejipanga kushinda kila mchezo ili kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi.

Simba ilirejea juzi Jumamosi kutokea nchini Misri ambapo walikuwa na kibarua cha kukamilisha ratiba kwa mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Al Ahly, uliopigwa usiku wa Ijumaa, ambapo Simba walipoteza kwa bao 1-0.

Sasa Simba inarejea katika ratiba ya michezo ya Ligi Kuu Bara, ambapo kesho Jumatano watakuwa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Simba inayokamatia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na pointi zao 46 walizokusanya baada ya kucheza michezo 20, wana nafasi ya kutwaa uongozi wa ligi kwa tofauti ya pointi saba iwapo watafanikiwa kushinda michezo yote minne ya Viporo waliyonayo, hivyo kufikisha pointi 58

Akizungumzia mipango yao, Meneja wa kikosi cha Simba Patrick Rweyemamu amesema: “Kikosi chetu tayari kimeanza rasmi kambi ya pamoja kwa ajili ya kujiandaa na michezo yetu ya Ligi Kuu Bara, hususani mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar siku ya Jumatano.

“Malengo yetu ni kuhakikisha tunafanya vizuri na kushinda michezo yetu yote ya Viporo ili kuwa na pointi zitakazotusaidia kuongoza msimamo wa ligi, na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa tulioutwaa kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita,”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic