April 20, 2021

 


SIMBA sasa wana jeuri tupu, na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo, wamekiangalia kikosi chao cha kwanza, wakafurahi sana na kusema: “Hakuna Yanga anayeingia first eleven ya Simba.

 

Simba wanatembea vifua mbele hivi sasa baada ya timu yao kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku wakiwa na asilimia kubwa pia ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya nne mfululizo licha ya Yanga kuendelea kuongoza ligi.

 

Baada ya kushinda jana dhidi ya Mwadui, Simba wamefikisha pointi 52, wakiwa nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi mbili tu huku Msimbazi wakiwac na viporo vitatu.

 

Kikosi cha kwanza cha Simba ambacho kimefanya maajabu msimu huu na ambacho kimekuwa kikitumika mara kwa mara kwenye mechi za kimataifa, kinaundwa na kipa Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Pascal Wawa, Joash Onyango, Taddeo Lwanga, Mzamiru Yassin, Luis Miquissone, Bernard Morrison, Clatous Chama na Chris Mugalu.

Hapo benchi kunakuwa na mashine nyingine kama Larry Bwalya, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Erasto Nyoni, John Bocco na wengineo.

Gumzo kubwa kwenye vijiwe vya mtaani ni mashabiki wengi wa Simba wanaamini hakuna mchezaji yeyote wa Yanga anayeweza kuingia katika kikosi chao cha kwanza, huku Yanga wakipinga kwa nguvu hoja hiyo Mjadala mkubwa kwa Yanga, ni kwamba wao wanaamini Mukoko Tonombe anaweza akapenya kuchukua nafasi ya Mzamiru Yassin, pia Saidoo Ntibazonkiza anaweza kucheza nafasi ya Mugalu huku pia Feisal Salum ‘Fei Toto’ akitajwa kuwa anaweza kucheza katika kikosi cha Simba.

 

Kufuatia ubishani huo, Championi Jumatatu,limewatafuta baadhi ya wachezaji wa zamani, viongozi na wachambuzi wa soka ambao nao wametofautiana katika mtazamo.

 

ALLY MAYAY (KIUNGO WA ZAMANI WA YANGA NA MCHAMBUZI WA SOKA)

“Kwanza inapaswa kueleweka kuwa soka la sasa linaongozwa na falsafa ya kocha na timu ambayo anaifundisha, hii ndiyo kwa kiasi kikubwa inaelekeza mahitaji ya wachezaji gani wanaweza kucheza kwenye kikosi chake.

 

“Falsafa ya Simba ni kumiliki mpira na kushambulia kwa nguvu ‘offensive’ hivyo sio wachezaji wote wa Yanga wanaweza kucheza kwenye kikosi cha Simba, lakini naamini kuna baadhi wanaoweza kucheza.

“Kwa uchache naamini Mukoko anaingia kikosini kwa kuwa yuko vizuri kimbinu na ana nidhamu ya mchezo, Saido pia anapata nafasi kutokana na uzoefu wake, na pale timu inapohitaji kushambulia kwa nguvu basi hata Tuisila Kisinda kama ilivyo kwa Luis Miquissone anaweza kutumika.”

 

ALLY KAMWE (MCHAMBUZI WA SOKA)

“Kwa upande wangu kwa ubora wa vikosi vyote viwili, naweza kusema ni mchezaji mmoja tu wa Yanga anayeingia kwenye kikosi cha kwanza cha Simba ambaye ni Mukoko Tonombe.“Mukoko ana uwezo wa kumtoa yeyote kati ya Jonas Mkude na Mzamiru Yassin.“Hii ni kwa kuwa tayari ameweza kuthibitisha kuwa ana uwezo wa kufunga mabaoanacheza kama kiungo ‘box to box’, lakini pia ana nguvu na mikimbio sahihi.”

 

AKIDA MAKUNDA (WINGA WA ZAMANI WA YANGA)

“Kwangu naamini ili mchezaji aweze kuingia katika kikosi cha kwanza cha timu ni lazima aweze kutengeneza muunganiko na wachezaji wengine atakaowakuta.“Hivyo naamini Mukoko, Saido wote wanaweza kucheza Simba, lakini pia hata Carlos Carlinhos ameonyesha kuwa ana jicho la pasi hivyo anaweza kushindania namba Simba.

ISMAIL ADEN RAGE (MWENYEKITI WA ZAMANI WA SIMBA)

“Mimi nitajibu swali hilo kama shabiki na mwanachama wa Simba, kama tunaangalia uwezo wa vikosi hivyo viwili kwa sasa basi nikuhakikishie kuwa, hakuna mchezaji yeyote wa Yanga anayeweza kupata nafasi Simba.

“Lakini pia ukiwachukua wachezaji wote wa Simba, basi pasi na shaka wote wanaweza kuingia ndani ya kikosi cha Klabu ya Yanga.“Simba ya sasa imekamilika kila idara, lakini kwa upande wa Yanga kunaonekana shida kubwa kwenye ushambuliaji na ulinzi, nadhani wanapaswa kuboresha maeneo hayo.”

STORI: JOEL THOMAS, Dar es Salaam

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic