April 4, 2021


 INASIKITISHA kuona ukanda wa Afrika ya Mashariki hakuna timu yoyote iliyofuzu kwenye michuano ya AFCON inayotarajiwa kutimua vumbi mwakani kule nchini Cameroon.

 

Timu za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini hakuna hata moja iliyofanikiwa kufuzu kwenye michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya taifa.

 


Jambo hili linashtua kwa kiasi kikubwa kuona ukanda wetu hakuna hata timu moja ambayo ilifanikiwa kufuzu kwenye michuano hii ambapo mwaka 2019 Kenya, Uganda na Tanzania zote zilifanikiwa kufuzu kwenye michuano hii.

 


Kwa upande wa Tanzania ambapo nitajikita zaidi kuzungumzia ni lazima tujiulize ni wapi tulikosea ili tuweze kurekebisha makosa kwa michuano ijayo, kwani baada ya kufuzu kwenye michuano hii mwaka 2019 kule nchini Misri ndoto ya Watanzania wengi ilikuwa ni kuona Stars inafuzu tena kwa mara ya pili.

 


Ilituchukua miaka 39 kufuzu michuano hii kwa mara ya pili, lakini mwaka mmoja mbele tumerudi tena kule tulikotoka ni jambo ambalo linatia simanzi kwa Watanzania wengi ambao walitamani kuiona tena bendera ya Tanzania kule nchini Cameroon.

 


Ni lazima kama tunahitaji kufanya vizuri kwenye michuano yoyote ni lazima kuwepo na mipango madhubuti ambayo itatufikisha kwenye nchi ya ahadi na si kuendelea kutiana moyo kila siku na tunaishia kuona wenzetu wakizidi kupiga hatua.

 


Hebu fikiria nchi kama Ushelisheli ambayo ilikuwa inafungwa hadi mabao sita na Tanzania inafuzu Afcon tena kwa matokeo bora kabisa, hapa ni wazi waliangalia ni wapi walikosea na wakaamua kufanyia kazi mapungufu yao yaliyojitokeza.

 


Mafanikio hayaji kwa miujiza ni lazima uweke mikakati na malengo thabiti kuhakikisha unayafikia, ni lazima ujiwekee na kuyaishi malengo kinachotokea leo Ushelisheli siyo bahati nasibu bali ni matunda ya kuyaishi malengo yao.

 


Nchi kama Cape Verde imekuwa jambo la mazoea kwao kufanya vizuri kwenye michuano hii na hii si kwa bahati mbaya bali waliamua kuyakubali mapungufu yao na kuyafanyia kazi, Cape Verde ni miongoni mwa mataifa ambayo yalikuwa nyuma kwenye mchezo wa soka lakini hawakukubali unyonge uwe sehemu ya maisha yao walijitathmini ni nini wanapaswa kufanyia na leo wanafurahia matunda ya malengo yao.

 


Ni lazima kama nchi tuhakikishe tunajiwekea malengo na kuyaishi kama kweli tunataka kufika mbali, kuna mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia ni lazima tuanzie hapa kuhakikisha kilichotokea kwenye mechi za kufuzu Afcon hakijirudii tena.



Tusiishi kwa ngekewa ni lazima tuishi kwenye malengo kama nchi, kuanza mikakati mapema na kuboresha mazingira ya kufanyia vizuri kwa kuhakikisha tunaiandaa timu kwa ajili ya kushindana na si kwa ajili ya kushiriki.

1 COMMENTS:

  1. Awe miweli, ana miaka mingapi? Umri nao ni kikwazo maana sisi waafrika huwa tunaficha sana age zetu

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic