LICHA ya kuuanza kwa matumaini makubwa msimu huu wa 2020/21, kwa kufanya usajili mkubwa wa kuboresha kikosi chao.
Huku mashabiki wao pia wakitimiza wajibu wa kujitokeza kwa wingi kwenda pale Terminal 3 ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, bado hali inaonekana kuwa tete ndani ya kikosi cha Yanga.
Kila mchezo wanaoshuka uwanjani kwenye Ligi Kuu Bara, ndivyo ambavyo matumaini waliyoanza nayo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, yanavyozidi kuyeyuka kwa mashabiki na wadau mbalimbali wa klabu hiyo.
Hali hii imepelekea kuwepo kwa manung’uniko mengi na lawama kutoka kwa mashabiki, ambao kila uchao wamekuwa wakitafuta nani wa kumlaumu kutokana na mwenendo wa kikosi chao.
Ukiwasikiliza leo watakwambia Waamuzi tatizo, kesho watakupa majina ya viongozi na wachezaji wanaowahujumu, lakini hata wakati mwingine kuwatupia zigo la lawama waandishi kwa madai ya kuisema vibaya klabu yao.
Hivi sasa viongozi wa Yanga wamekuwa na kazi kubwa ya kuwatuliza Wanachama na kuwapa moyo juu ya kesho bora ya klabu hiyo. Naupongeza uamuzi huo wa uongozi, kwa kuwa klabu hiyo kwa sasa inahitaji kuwa pamoja kuliko kipindi chochote kile.
Nawaelewa mashabiki wa Yanga ambao wanaonekana kuja juu pale inapotokea kikosi hiko kinapoteana uwanjani, kwani bila shaka watakuwa wanazikumbuka zile sauti za baadhi ya viongozi wao, wakiwaamrisha kutengeneza mistari kama Wanajeshi wanaojiandaa na Gwaride la heshima mbele ya Rais, pale Terminal 3.
Wengine wanachoka zaidi wanapoukumbuka ule msafara wa rekodi wa kumpokea kiungo mshambuliaji wao wa kimataifa raia wa Angola, Carlos Fernandes ‘Carlinhos’, ambaye ilibidi atembezwe kwenye gari la wazi ili Wanayanga wengi zaidi wapate nafasi ya kumuona wakati anawasili.
Bila shaka haya ni baadhi ya mambo yanayowapa hasira zaidi Wanachi kwa sasa.
Hali ya maendeleo ya Yanga kwa sasa inatia shaka, si kwa Wanachama wa Yanga pekee, bali hata kwa wapenda michezo kiujumla. Afya ya soka letu inategemea kwa kiasi kikubwa katika ushindani wa Simba na Yanga.
Sasa katika hali ya sasa ambapo Simba inazidi kuwa bora kila siku na kutandaza utawala wake, ilipasa kuiona Yanga pia ikionyesha misuli na kuipa changamoto Simba na sio kuacha utawala huu ambao umedumu kwa misimu mitatu sasa uendelee.
Viongozi wa Yanga kwa kushirikiana na Wanachama wao wanapaswa kuja na njia ya kupindua meza na kuhakikisha wanaijenga tena klabu yao na kuirejeshea uimara wao wa asili.
Na katika hili hatua za haraka
sana zinapaswa kuchukuliwa, kwani iwapo Yanga watakosea ‘Step’ tu basi itabidi
wasahau kuhusu kushindana na Simba siku zijazo.
Uchambuzi wa Edibly Lunyamila mchezaji wa zamani wa klabu ya Yanga na Taifa Stars.
Kumbuka unaweza kuupata uchambuzi huu kupitia gazeti la Championi kila Jumatatu.
0 COMMENTS:
Post a Comment