TIMU nne kwa sasa rasmi zitawakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa ambayo yanaandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, (Caf).
Kwa kuwa imekuwa wazi kwamba ni timu nne ambazo zitaipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa basi nina amini kwamba zile ambazo zitapata nafasi zina kazi ya kufanya kufikia mafanikio.
Msimu uliopita tulipoteza nafasi hiyo adimu baada ya timu shiriki kushindwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ambayo yanaushindani mkubwa.
Kwa kuwa kila timu inahitaji kuwakilisha Tanzania kimataifa basi maandalizi yaanze kwa umakini wakati huu ili kuwe na matokeo chanya wakati ujao.
Tanzania ina nafasi mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na nafasi mbili ni kwenye Kombe la Shirikisho basi ni lazima kila timu itakayopata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa lazima ifanye kweli.
Hakuna mchezo ambao utakuwa mwepesi kwa timu hizi ambazo zitapata nafasi kushiriki mashindano ya kimataifa. Imani yangu ni kwamba watakaopata nafasi watafanya vizuri.
Jambo linalotakiwa ni maandalizi mazuri hakuna jambo lingine kwani wakati uliopita tulichezea nafasi hizi kwa kuwa hakuna timu iliyoweza kufika mbali.
Kwa msimu huu tunaona kwamba timu ambazo zilipatata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa zilitimiza majukumu yao kwa ukamilifu.
Namungo licha ya kwamba ulikuwa ni msimu wao wa kwanza kushiriki mashindano ya kimataifa waliishia hatua ya makundi ikiwa ni kubwa kwao.
Ukweli ni kwamba Namungo licha ya kupenya hatua ya makundi walianza kuonyesha mwanga wa kupambana ila mambo yakawa magumu kwao hatua ya makundi.
Jambo ambalo walishindwa kulifanyia kazi waliweka wazi kwamba ni kukosa uzoefu katika mashindano hayo hivyo nina amini kwamba timu nyingine zimejifunza jambo kupitia kwao.
Kushindwa kupata pointi kwenye mashindano ya kimataifa pamoja na kushindwa kufunga bao hatua ya makundi ilikuwa mbovu hivyo watakaofuata wanapaswa kuivunja kabisa.
Mabingwa watetezi Simba wao waliweza kutinga hatua ya robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwa kufanya hivyo wanastahili pongezi kwa kuwa walikuwa hawapewi nafasi ya kufanya vizuri mwisho wa siku wakafanikiwa.
Kwa kuwa wanauzoefu na wanajua namna mashindano yalivyo imani yangu ni kwamba ikiwa watapata nafasi kushiriki mashindano ya kimataifa watapeperusha vema bendera ya Tanzania kimataifa.
Suala lao la kujiamini kupita kiasi nina amini kwamba litafanyiwa kazi na watapambana wakijua kwamba wanamalengo gani kimataifa.
Kila kitu kinawezekana ikiwa maandalizi yatakuwepo kwa timu zote kwa kuanza kutafuta wachezaji ambao wataweza kuendana na mfumo ama kuwa na wachezaji wenye shauku ya kufanya vizuri kimataifa.
Tunakumbashana kwamba kwa sasa ligi ipo kwenye hatua ya lala salama ikiwa ni mzunguko wa pili na timu zinapambana kupata kile ambacho wanastahili.
Ikiwa hesabu zitagoma wakati huu kwenye mechi zilizobaki hakuna kitakachotokea kipo wazi ni timu kushuka daraja moja kwa moja na huko kazi ni kubwa kusaka nafasi kurudi kwenye ligi.
Zipo ambazo zimeonekana kuzinduka wakati huu wa lala salama hii ni mbaya kwao kwa kuwa wanacheza kwa presha kubwa tofauti na awali ligi ilipoanza.
Itapendeza wakati ujao kwa timu zote kuanza kupambana kwenye mechi zijazo mwanzoni na hiyo itafanya ushindani kuwa mkubwa mwanzo mwisho.
Kila timu inahitaji kushinda kwenye mechi zake lakini ukweli ni kwamba mechi ambazo zimebaki kwa sasa ni chache na ikiwa timu itapoteza mechi moja basi itazidi kujihatarisha kuwa kwenye nafasi ya kushuka.
Kushiriki Ligi Daraja la Kwanza kunahitaji akili nyingi kujinasua hapo kwa kuwa zilizotoka Ligi Kuu Bara rekodi zinaonyesha kwamba hazina bahati ya kupanda zaidi ya kushuka mpaka Ligi Daraja la Pili.
Hivyo basi rai yangu ni kwa zile ambazo zimepanda kuona namna ambavyo zitapambana kwenye kusaka pointi tatu kwenye mechi ambazo watacheza wakati ujao.
Kikubwa kinachotakiwa kwa mechi hizi za lala salama ni timu kucheza kwa umakini kwenye kusaka pointi tatu na mwisho wa mzunguko wa pili hapo itafahamika nani amevuna nini mwisho wa msimu.
0 COMMENTS:
Post a Comment