July 28, 2021

JULAI 9, mwaka huu inawezekana ikawa ndiyo siku mbaya zaidi kwenye maisha ya mchezaji wa klabu ya soka Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdam. Hii ni baada ya baada kutokana na kuhusika kwenye ajali mbaya ya gari akiwa pamoja na kikosi cha klabu hiyo kilichokuwa kikitoka mazoezini.

Polisi Tanzania walipata ajali hiyo wakiwa wanatoka mazoezini katika viwanja vya TPC Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar baada ya gari walilokuwa wamepanda kuacha njia, na kugonga mti eneo la Mkababuni.

Kupitia ajali hiyo mbaya wachezaji mbalimbali walipata majeraha makubwa, na madogo huku mchezaji aliyeonekana kuwa kwenye wakati mgumu zaidi akiwa ni Mdamu ambaye alivunjika miguu yake yote miwili na kupelekea kufanyiwa upasuaji.

 

Ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa hakukuwa na mchezaji wala kiongozi wa Polisi Tanzania ambaye alipoteza maisha kwenye ajali hiyo licha ya kwamba, kisaikolojia wengi wao waliathirika kwa namna moja au nyingine.

 

Kutokana na changamoto hiyo, wadau mbalimbali wa michezo zikiwemo klabu, viongozi wa michezo na wale wa kiserikali kutuma salamu za pole katika jitihada za kuwafariji, kutokana na changamoto hiyo kubwa waliyoipata.

 

Lakini nitoe pongezi kwa wadau mbalimbali ambao waliona uhitahi wa kuchangia chochote kitu kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya mdamu. Bilas haka kwa matoleo hayo ya hali na mali ikiwemo maombi kwa wale wenye Imani zao. Huo ndio utu tunaouzungumzia jambo ambalo linafaa kuendelezwa kila siku miongoni mwa wenzetu wanaokumbana na changamoto mbalimbali.

 

Mdamu kwa sasa amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoka katika Hospitali ya KCMC alikokuwa amelazwa hapo awali, ambapo Uongozi wa Polisi umeweka wazi kuwa lengo la kufanya hivyo ni kumsogeza karibu na familia yake wakati akiedelea kuwa kwenye matibabu. Kwa sasa anaendelea vizuri hali yake na amelazwa MOI.

 

Huku ikitegemewa kuwa pale maendeleo ya afya yake yatakapokua yameimarika, atahamishiwa katika hospitali ya Polisi iliyopo Kurasini kwa ajili ya kuendelea kupata matibabu mengine ya kawaida.

 

Lakini katika hali ya kushangaza sana hivi karibuni kumeibuka sintofahamu kubwa juu ya tuhuma kutoka kwa baadhi ya Wanafamilia ya Mdamu ambazo zinaeleza kuwa, Uongozi wa Polisi Tanzania unaonekana kumtelekeza mchezaji huyo kwa kutolipia huduma za matibabu ambayo nyota huyo anayahitaji, lakini pia kutoenda kumwona.

 

Hali hii iliusukuma uongozi wa Polisi Tanzania kupitia kwa Ofisa Habari wake, Hassan Juma ameeleza yafuatayo: “Ubinaadam ni kazi, nimetoka asubuhi kumuona Mdamu Muhimbili na toka tumemhamishia Muhimbili sijawahi kukutana na mwanafamilia zaidi ya kaka yake.

 

“Klabu itaendelea na matibabu katika mfumo uleule tulioelekezana wa kutunza risiti pale itakapohitajika kipimo chochote au dawa wakati sisi hatupo tutarejesha fedha walizotumia kulingana na gharama za risiti.

 

“Suala la kukaa muda wote hospitali kwetu viongozi ni ngumu, lakini yupo daktari wa Hospitali ya Polisi Dar es Salaam ambaye hufika kila siku kujua maendeleo ya mgonjwa.

 

“Huwezi kumleta Mwenyekiti au katibu wakati watendaji wengine wapo. Hata tulipokuwa Moshi pale walipotoa pesa mfukoni mwao walituma risiti nasi kurejesha Amana waliyotumia na tuna ushahidi wa miamala hiyo.

 

“Pia ieleweke kiasi cha Shilingi 50,000 anayopewa siyo kwa ajili ya dada, au ndugu bali tuliona kila baada ya siku nne apewe hiyo kwa ajili ya chakula katika jitihada za kuisaidia familia katika jukumu hilo, kwani stahiki zote za kimkataba anapewa na klabu yake.

 

“Shida dada mtu alitaka klabu imtunze nae kwa madai ya kuwa tegemeo lake, jambo ambalo imekataa na hilo ndiyo chanzo Cha yote. Mkihitaji risiti na miamala yote tangu Moshi Hadi Sasa tunaweza kuwaonyesha ili kujua ukweli wa hili. Klabu itawajibika kumtunza mchezaji wetu ambaye ndiye mwajiriwa na siyo familia ya mchezaji.”

 

Ukifuatilia maelezo haya ya pande zote mbili, utagundua kuwa katika hili inaonekana wazi kuna mazingira ya baadhi ya watu kutaka kujinufaisha kutokana na changamoto hii, jambo ambalo linaweza kuleta athari kubwa kwa Mdamu.

 

Chondechonde naomba hili lisipewe nafasi hata kidogo tushikamane kuokoa maisha ya soka ya Mdam, na kuachana na roho za tamaa katika hili.


Uchambuzi wa Vuvuzela kwenye gazeti la Championi Jumatano 

1 COMMENTS:

  1. Hivi wachezaji hawa hawana bima? Nashauri tff na uongozi wa police fc watoe utaratibu tujitahidi kuchangia.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic