KOCHA wa Klabu ya Atletico Madrid ya Hispania, Diego Simeone amesaini kandarasi ya miaka mitatu kuendelea kukinoa kikosi hicho chenye maskani yake jijini Madrid mpaka mwaka 2024.
Simeone aliyekuwa anakaribia kumaliza kandarasi yake na mabingwa hao wa La Liga 2020-21, amesaini mkataba huo pamoja na jopo lake zima akiwemo kocha msaidizi, Nelson Vivas, kocha wa magolikipa, Pablo Vercellone na makocha wa utimamu wa mwili, Hernan Bonvinvini na Oscar Ortega.
Siri ya kocha huyo mzaliwa wa Argentina kusaini kandarasi hiyo ni mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa na klabu hiyo tokea ajiunge nao Januari 1, 2012 akitokea klabu ya Racing pamoja ya yale ya msimu uliopita wa kuwa mabingwa wa La Liga mbele ya vigogo Real Madrid na Barcelona.
Diego ndiye kocha pekee aliyefanikiwa zaidi kwenye historia ya klabu hiyo kwa kuiongoza kutwaa mataji mengi, mataji 8 yakiwemo ya La Liga mara 2, mwaka 2013-2014 na 2020-2021, Europa Lague mara 2, mwaka 2011-2012, UEFA Super Cup mara 2, mwaka 2012 na 2018, Copa del rey mwaka 2013 na Supercopa de Espana 2014.
Mafanikio hayo yamemfanya kocha huyo mwenye mizuka mikali awapo benchini kushinda tuzo kubwa mbalimbali zikiwemo za kuwa kocha bora wa La Liga mara tatu 2012-2013, 2013-2014 na mwaka 2015-2016, kocha bora wa Ulaya 2011-2012 na kocha bora wa mwaka 2016 iliyotolewa na Shirikisho la soka la kimataifa la Historia na takwimu IFFHS.
Tuzo kubwa aliyeipata kocha huyo akiwa na Atletico Madrid inabaki kuwa ile ya mshindi wa tuzo ya kocha bora wa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2011-20 ambazo pia ilitolewa na Shirikisho la soka la kimataifa la Historia na takwimu IFFHS.
Kabla ya kusaini mkataba huo tayari Diego alikuwa kocha pekee kwenye historia ya La Liga kuiongoza klabu moja kwenye misimu mingi zaidi, misimu 8 tokea ajiunge na Atletico Madrid Januari 1, 2012 akitokea klabu ya Racing hivyo mkataba huo utazidi kumfanya atanue rekodi hiyo zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment