WAKATI umewadia na muda umebaki
mchache sana kabla ya watani wa jadi
kuvaana kwenye Uwanja wa Lake
Tanganyika mjini Kigoma.
Historia inakwenda kuandikwa kwa uwanja
huo kuwakutanisha watani wa jadi Yanga na
Simba katika mechi muhimu ya fainali ya
Kombe la Shirikisho.
Fainali ambayo imo katika rekodi ya
kuwakutanisha watani wa jadi kucheza
mechi mbili ndani ya mwezi mmoja na hapo
hakuna mechi ya kirafiki.
Mwezi huu wa Julai, tayari Yanga
wamemfunga Simba kwa bao 1-0 katika
mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo iliihakikishia
Yanga kusimama katika nafasi ya pili ya ligi
hiyo lakini ikaizuia Simba kuchukua ubingwa
mapema, mikononi mwa watani wake
Yanga.
Hii ni mechi ya pili, mechi ambayo Yanga
wanalitaka Kombe la shirikisho, wanataka
kumvua Simba ubingwa na kuthibitisha
ushindi wao katika mechi iliyopita wala
haukuwa wa kubahatisha.
Kwa upande wa Simba, wanataka kutetea
ubingwa wao, wanataka kulipa kisasi na
tatu kuonyesha Yanga waliwaotea katika
mchezo ule ambao wengi hawakutarajia
kuona Simba wanapoteza.
Wakati hayo yanakwenda kutokea na
matokeo tukisubiri dakika 90 za mchezo
huo, niwakumbushe waamuzi kwamba
mwamuzi wa mchezo uliopita Emmanuel
Mwanembwa alileta shida kubwa ambayo
imeacha malalamiko.
Shida hiyo ilikuwa wazi na ilionekana ni
kama mwamuzi alipanga kumaliza mchezo
huo bila ya kutoa penalti au kutoa kadi
nyekundu hata kama ilitakiwa.
Tuliona rafu kadhaa ambazo wakati
mwingine tungeweza kusema zilistahili kadi
nyekundu kabisa. Lakini mwamuzi hakutoa
hata kadi ya njano ikionekana wazi alipania
kuubalansi mchezo.
Kulikuwa na penalti, kila mmoja aliona lakini
mwamuzi hakutoa pigo la penalti na hii ni
ile sehemu ya kuonyesha kwamba
kunakuwa na mwenendo au mwelekeo wa
kisiasa unaotokana na ukubwa wa mechi ya
Yanga na Simba, waamuzi hawapaswi
kuingia huku.
Kama ni kadi, basi mtu ale kadi na kama ni
penalti basi mara moja itolewe kwa mujibu
wa sheria 17 za mchezo wa soka. Lakini
haikuwa hivyo ndio maana nimeamua
kumkumbusha mwamuzi Ahmed Arajiga na
wenzake kwamba mechi wanayokwenda
kuchezesha ni dhamana kubwa na ndio
inabeba thamani yote ya michuano ya
Kombe la Shirikisho ambayo Azam Media
wamewekeza mamilioni ya fedha. Wengine
wamewekeza kwenye timu na zimetoa ajira
kwa wachezaji maelfu.
Waamuzi walioteuliwa kwa ajili ya kucheza
mchezo huo ni pamoja na Ahmed Arajiga
(Manyara) ambaye atasaidiwa na Ferdnand
Chacha (Mwanza) na Mohammed Mkono
(Tanga) wakati mwamuzi wa akiba atakuwa
ni Elly Sasii wa Dar es Salaam.
Si jambo zuri mtu kufanya uzembe tena kwa
zile siasa za kuhofia au kutaka
kuwafurahisha baadhi. Au kutaka
kutoonekana haukuwa mkatili au
haukuboronga na hapa unakuwa
umezikanyaga sheria 17 za mchezo wa soka
na mwisho lawama kama ilivyo ada
zinaangushiwa kwa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), jambo ambalo si sahihi.
Waamuzi wawe imara na wakumbuke kama
watafuata weledi wa kazi yao na uamuzi
wao uwanjani ukawa ni ule ambao ni sahihi.
Basi hakuna kitakachoweza kuwaangusha
au kuwafanya waonekane walikosea hata
kama itakuwa ni baada ya miaka 100 ijayo.
Ukweli haupingiki, ukweli haushindwi milele
na vizuri kufanya sahihi na kuacha kuwe na
malumbano na kadhalika, lakini mwisho
hakuna anayeweza kukushinda.
Bila shaka, hii imekuwa ni tabia kwa muda
mrefu kwamba waamuzi wanaingia
uwanjani kuchezesha mechi ya watani
wakiwa wanataka kuhakikisha inaisha bila
kadi nyekundu au kutoa penalti. Wako
waamuzi hufurahia hata mechi iishe kwa
sare kwa kisingizio cha kupunguza
“makelele”.
Suala la “makele” si kazi yao, nani
atachukizwa au nani ataumizwa kwa
kupoteza au yupi atafurahi kwa kushinda,
waamuzi waitoe kabisa hiyo badala yake
waende kuchezesha mpira tu na suala la
matokeo, litokane na mchezo
utakavyokuwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment