AGOSTI 15, 2021 kikosi cha Yanga kiliondoka hapa nchini kuelekea Afrika Kaskazini, kwenye nchi ya Morocco kwa ajili ya kuweka kambi iliyotarajiwa kutumia siku kumi kwa ajili ya maandalizi ya kabla ya msimu ‘Pre season’, ambapo baada ya safari ya siku mbili walitua Jijini Marrakech Agosti 17, ambapo walianza rasmi mazoezi.
Kambi hiyo ilihusisha wachezaji wote wa Yanga ambao watatumika msimu ujao wakiwemo nyota wapya kumi ambao wamesajiliwa kwenye dirisha kubwa la usajili ambalo litafungwa rasmi Agosti 31, mwaka huu.
Leo ifikapo saa sita usiku, dirisha la usajili litafungwa kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF).
Baada ya siku sita za programu ya mazoezi hayo ambayo yalikuwa yakiwasilishwa kwa wapenzi na wadau wa Yanga kupitia mitandao ya kijamii ya klabu hiyo, ghafla kambi hiyo ilivunjwa.
Taarifa rasmi kutoka kwenye Uongozi wa Yanga zilieleza kuwa kutokana na sababu mbalimbali na kwa maslahi mapana ya klabu hiyo uongozi uliamua kusitisha kambi hiyo na kueleza wazi kuwa kikosi kitakuwa Avic Town, Kigamboni kwa ajili ya muendelezo wa kambi hiyo.
Hapo mwanzo Yanga walitarajia kusalia Morocco mpaka Agosti 27, ambapo wangerejea nchini na kufanya mazoezi mepesi ya kujiandaa na mchezo wao wa kilele cha siku ya Mwananchi dhidi ya Zanaco uliochezwa Agosti 29, Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ni jambo lililowazi kuwa tangu taarifa rasmi ya kuvunjwa kwa kambi ya Yanga zitolewe kumekuwa na maswali mengi zaidi kwa wadau wa soka kulinganisha na majibu waliyonayo. Bila shaka hali hii inatokana na kutokujitosheleza kwa maelezo yaliyotolewa kama sababu za kufanya hivyo.
Sababu mbalimbali zimetolewa kutoka kwa watu wa karibu wa Yanga kuhusiana na kuvunjwa kwa kambi hiyo, ambapo wapo wanaosema kuwa hali ya joto iliyokuwepo huko Marrakech ni sehemu ya changamoto zilizopelekea kuvunjwa kwa kambi hiyo, ambapo inaelezwa kuwa joto ni kubwa kulinganisha na lile lililokuwepo hapa Dar es Salaam.
Lakini kama ni kweli hii ndiyo sababu swali ni je, kwa nini iwe ghafla? Wakati tayari timu hiyo imeweka kambi kwa siku sita na katika kipindi hicho timu ilikuwa inaendelea na mazoezi bila shida hiyo kutipotiwa hapo awali. Lakini pia inawezekanaje waratibu wa kambi hii wasilijue hili kabla na kufanya marekebisho ya mahali pengine kwa kuweka kambi kwa kuwa kwa sasa zipo njia nyingi za kuweza kutambua hali za hewa za sehemu hizo, bila shaka unaweza kuona ni kwa nini sababu hii inaleta mashaka.
Wapo wanaosema, Yanga imelazimika kuvunja kambi ili kuwahi tamasha lao la wiki ya Mwananchi lililofanyika Agosti 29, mwaka huu. Sababu hii pia haiwezi kuwa na mashiko kwa kuwa tayari uratibu wa safari uliweka wazi kuwa timu ingeondoka Agosti 27 ili kuwahi tamasha hilo.
Hili lilipangwa tangu mwanzoni mwa safari, na sioni Uongozi wa Yanga ukivunja kambi kwa ajili ya tukio hili, labda kama walihofia taratibu za usafiri katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na vikwazo vya hapa na pale kusafiri kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine kutokana na taratibu za vipimo za maradhi ya UVICO-19.
Lakini pia zipo taarifa zinazoeleza kuwa uongozi umefikia maamuzi hayo kutokana na uhalisia kuwa sehemu ya wachezaji wa kikosi hicho walitarajiwa kuondoka ili kujiunga na kambi za timu za mataifa yao kwa ajili ya michezo ya kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya kombe la dunia 2022.
Lakini sababu hii pia haiwezi kuwa na mashiko kwa kuwa tayari ratiba ya michuano hii ilikuwa ikijulikana tangu awali na hata wakati Yanga wanaondoka walikuwa wakijua wapo baadhi ya nyota wao ambao wangepaswa kuondoka kambini kwa ajili ya kujiunga na vikosi vya mataifa yao na uongozi ulipaswa kujiandaa na hilo.
Sawa Yanga wamekaa siku sita Morocco, lakini swali gumu zaidi ni je, kocha wa Yanga amepata kile ambacho alikitarajia katika kambi hiyo? Je, ni kweli huo ni muda wa kutosha kwa mwalimu kukamilisha programu aliyoiandaa? Lakini kwa kuwa kambi hii ilikuwa ikigharamikiwa na kiasi cha fedha za uhamisho wa Tuisila Kisinda kwenda RS Berkane je, kuna malipo yoyote watayapata Yanga kama sehemu ya thamani ya Kisinda?
Wakati maswali yakiwa mengi bado tumeshuhudia pia kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Zanaco namna matundu yalivyokuwa kwa Yanga baada ya kupoteza kwa kufungwa mabao 2-1.
Uongozi wa Yanga wenyewe umebainisha kwamba umeyaona matundu na utayafanyia kazi hivyo ni muhimu kuona kwamba wanafanya kazi kweli ili wapate matokeo mazuri katika mechi ambazo watashiriki ikiwa ndani ya Ligi Kuu Bara pamoja na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nyuma pale kati panavuja
ReplyDeleteOnyango?
DeleteIkiwa sababu ni joto, jee joto hilo lilikuwa kwa timu hiyo tu na wala si kwa Simba ambao waliendelea na kucheza mechi mbili bila ya woga
ReplyDeleteUlishaambiwa wako maeneo tofauti. Joto la Moshi ni sawa na la Arusha?
DeleteKwa hiyo walikurupuka tu wakaenda bila kujua wanakoenda hali ya hewa ikoje... Utopolo bado sana
DeleteMngesubiri kule Moroco na kuyatimiza mlioyaendea, kulekule mngejuwa ubovu upo wapi mkarekebisha halafu mngewasha tena mitambo kurakibisha kila kitu. Gharama ya mamilioni yaliyopotea bure mngelipata zaidi ya nyota wane wa nje
ReplyDelete