IKIWA zimebaki siku mbili kwa dirisha kubwa la usajili kufungwa, Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) limekomelea msumari kwamba halitaongeza muda wa siku za usajili kwa timu ambazo hazitafanikisha suala hilo.
Dirisha la usajili lilifunguliwa Julai 19 na linatarajiwa kufungwa Agosti 31 kwa klabu za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza kwa sasa inaitwa Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema kuwa kila siku wamekuwa wakiwasisitiza watu wenye timu kufanya usajili kwa wakati kwa kuwa hakuna muda wa kuongezwa.
“Ipo wazi kwamba hatutaongeza muda kwa ajili ya kufanya usajili kwa timu zote. Siku zote tumekuwa tukiwasisitiza waweze kufanya usajili kwa wakati kwani katika hilo kanuni zipo wazi na zinaeleza.
“Tunawasisitiza kusajili kwa wakati kwa timu zote, pia kwa wale ambao wanasajili wachezaji wa kimataifa ni lazima kukamilisha uhamisho wa wachezaji wao, (ICT) ili waweze kuwatumia,” amesema Ndimbo.
Kwa sasa timu zote bado zipo kwenye usajili ikiwa ni pamoja na DTB inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ikiwa imeweza kupata saini ya nyota waliowahi kucheza ndani ya Ligi Kuu Bara ikiwa ni pamoja na Juma Abdul, Amiss Tambwe.
Pia Yanga na Simba nazo kama kawaida zimefanya usajili sawa na Kagera Sugar ya Bukoba na Namungo FC pia wameshusha mashine ikiwa ni pamoja na Obrey Chirwa aliyekuwa mchezaji huru baada ya kumaliza dili lake ndani ya Azam FC.
0 COMMENTS:
Post a Comment