TUNA timu nne kutoka Tanzania ambazo zitapeperusha bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa hili sio jambo dogo ni kubwa.
Ikiwa hesabu za wawakilishi hawa ni kufanya mambo katika hali ya kawaida hapo matatizo yanaanzia hapo. Timu ikianza jeuri muda huu kinachofuata ni anguko.
Kila mmoja kuanzia mashabiki, wachezaji na benchi la ufundi wanahitaji kuona jambo likitokea kwa timu zao kupata matokeo chanya ndani ya uwanja.
Haitawezekana kupatikana matokeo chanya ikiwa kila mmoja anafanya vile anavyohitaji. Kujiona kwamba mnaweza kufanya vizuri na kuendelea kujigamba haina maana.
Kikubwa ambacho kinahitajika kwenye mashindano ya kimataifa ni kupenya kwenye hatua ambazo timu itapita. Jambo la msingi ni kupata ushindi.
Yanga na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam FC pamoja na Biashara United kwenye Kombe la Shirikisho hapo kazi ni kubwa kwa kila mmoja katika kusaka mafanikio.
Ni maisha ya mpira kwa kuwa kila timu inapoingia uwanjani inahitaji kupata ushindi na hakuna kocha ambaye anafikiria kushindwa hilo lipo wazi.
Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi itaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.
Kupata nafasi ya kuipeperusha bendera kwenye mashindano ya kimataifa haipaswi kwenda kinyonge. Wawakilishi wa kimataifa ni lazima mfanye kweli haswa.
Anguko la timu moja litawafanya wengine nao kushindwa kufurukuta mbele ama kupoteza kabisa nafasi ya kuwa na timu nne wakati ujao.
Ukiwatazama Simba wakati uliopita walitinga hatua ya robo fainali hii inapaswa pongezi. Wakibweteka kama zama zile za UD Songo wataonja joto ya jiwe.
Kwa sababu wakati ule walipoweza kutinga hatua ya robo fainali waliona kwamba wanaweza kufanya vizuri tena wakati mwingine. Hakuna wepesi kazi ipo palepale.
Ikiwa wataingia tena kweye mashindano ya kimataifa na mtazamo kwamba wao ni wakubwa anguko lipo njiani tena kama kawaida yao kuamua kucheza kwa mazoea.
Matumaini yangu wamiliki wa timu, wachezaji pamoja na wamiliki wa timu wanaona namna mambo yanavyokwenda hivyo wataongeza umakini wakati watakapokuwa kwenye ushindani.
Ukiachana na mashindano ya kimataifa pia kuna suala za mechi za Ligi Kuu Bara. Ligi Daraja la Kwanza ambayo kwa sasa inaitwa Champinship. Zipo nyingine pia zimepanda kushiriki Ligi Kuu Bara.
Tunataka kuona timu ikipanda kwenye ligi iwe na uwezo na vigezo vya kuhimili mikikimikiki ya huku kwani hakuna kuzubaa ni mwendo wa kukimbizana kila saa.
Mbali na ligi kuu ya wanaume pia kuna Ligi ya Wanawake hapa pia kuna umuhimu wa kuitazama kwa ukaribu ili kutengeneza timu makini pia kwa wanawake.
Kutokana na ushindani uliopo hasa kwenye timu za wanawake kuna umuhimu wa wadau kujitokeza pia kutoa sapoti kwa wanawake ili nao pia waweze kuleta ushindani.
Tumeona kwamba hadi huku masuala yao ya usajili ni vita kubwa jambo linaloonyesha kuwa kuna mwamko ambao unaanza kuonekana mpaka huku hivyo wadau ni muhimu kuzipa sapoti.
Simba Queens ilifanikiwa kutwaa ubingwa msimu uliopita na iliweza kupata ushindani mkubwa kutoka kwa Yanga princess.
Kikubwa ambacho wadau wanapaswa kukitambua ni kwamba huku pia sapoti yao ni muhimu kwa kuwa kila mchezaji anaonyesha kiwango bora akiwa ndani ya uwanja katika kupambania matokeo.
Kuna umuhimu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutazama namna ya kuwapiga tafu wachezaji pamoja na timu kiujumla kwani wengi hali zao bado hazijawa sawa.
Kwa msimu mpya nina amini kwamba kutakuwa na maboresho kwa kila timu ambapo zitakuwa zimetumia usajili kufanya maboresho ndani ya timu zao.
Wachezaji nao wanapaswa wajitume wawapo uwanjani kwani inawapa nguvu na kuwaongezea thamani yao ndani ya uwanja ili kuweza kuwaongezea thamani pale wakati wa masuala ya usajili inapofika.
Timu chache zina uhakika kuhusu posho na stahiki za wachezaji na hii ni mbaya kwani mambo yakiwa hivi ushindani utazidi kupungua.
Ili kuwa na timu ya taifa imara ni lazima kujenga timu bora ambazo zitashiriki ligi na ziwe katika ushindani wa kweli muda wote jambo litakalofanya mwalimu awe na chaguo bora katika kujenga kikosi chake.
Wakati uliopo kwa sasa kwa ajili ya msimu mpya wa 2021/22 timu zote zinapaswa zijiandae ili kufanya vizuri. Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) pamoja na wadau kutazama namna mpya ya kuendelea kutoa sapoti kwa wanawake.
Hakuna muda wa kuzubaa kwa sasa ni muda wa maandalizi ikiwa itakuwa tofauti na matokeo pia yatakuwa tofauti. Kwenye mpira hakuna uchawi ila ni maandalizi.
0 COMMENTS:
Post a Comment