February 24, 2013




Kama unakumbuka Mtibwa Sugar ndiyo waliokuwa wa kwanza kuwafunga Simba katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Baada ya kuwafunga kwa mabao 2-0 mjini Morogoro, tafrani kubwa likazuka mashabiki wakitaka kipa Juma Kaseja na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ waondoke.

Baada ya hapo, Simba ikapoteza mechi ya pili dhidi ya Toto African kwa kufungwa bao 1-0, safari hii nyumbani Taifa.
Tokea kuanza kwa mzunguko wa pili, Simba haijapoteza hata mechi moja, kwani baada ya kucheza nne, imeshinda mbili na sare mbili. Sasa inakutana tena na Mtibwa Sugar, nini kitatokea?

Inawezekana kwa Simba kukubali kuwa wateja wa Mtibwa Sugar msimu huu? Au ndiyo wakati mwafaka kwa mabingwa hao watetezi kulipa kisasi kwa ‘Wakata miwa’ wa Manungu?
Hakuna ubishi mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa kati ya timu hizo mbili, hakuna kikosi legelege ingawa Mtibwa iliwashangaza wengi hivi karibuni, kwani baada ya kuwakomalia Yanga kwa sare ya bao 1-1, ikalala kwa Azam FC kwa mabao manne!

Katika mechi ya leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar. Mtibwa Sugar iliyo katika nafasi ya saba na pointi 24, itakuwa inapambana kukwekea juu wakati Simba yenye 31 inataka kuifukuza Azam FC yenye 36.

NGOME
Ngome ya Mtibwa imeruhusu mabao 18 ambayo ni mengi zaidi ya ngome ya Simba ambayo imefungwa mabao 14.

USHAMBULIAJI:
Simba imefunga mabao 26, huku Mtibwa ikiwa imepata 20 tu hali inayoonyesha Msimbazi ni imara zaidi kama litakuwa ni suala la takwimu.
Lakini bado Mtibwa Sugar inaonekana ni moja ya timu zinazoonyesha soka la uhakika ikiwa chini ya wazalendo Mecky Maxime, Zuberi Katwila na Patrick Mwangata wakati Simba inayonolewa na Mfaransa Patrick Liewig akisaidiwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ bado haijaonyesha kiwango kinachowaridisha mashabiki wake.

Dakika 90 za leo ndiyo zitatoa matokeo lakini iwapo mshambuliaji Felix Sunzu atakuwa amepona na kuongeza nguvu basi Simba itakuwa hatari zaidi wakati Hussein Javu na Shaban Kisiga ni wachezaji wa kuchungwa sana na walinzi wa Simba, la sivyo watalia.

Kipa wa Mtibwa Sugar, Casillas huenda akawa mmoja ya wachezaji kivutio kutokana na umahiri ambao amekuwa akiuonyesha hivi karibuni katika mechi mbalimbali za ligi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic