Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Fat
na baadaye TFF, Michael Wambura amesema iwapo Tanzania itafungiwa na Shirikisho
la Soka la Kimataifa (Fifa), anayepaswa kulaumiwa ni Rais wa shirikisho hilo,
Leodeger Chilla Tenga.
Wambura amesema matatizo
yaliyojitokeza wakati wa upitishwaji wa katiba mpya ya TFF iliyokataliwa na
serikali yalitokana na usimamizi mbovu wa shirikisho hilo.
Akizungumza leo na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam, Wambura alisema Tenga ndiye atakuwa wa kulaumiwa
kama kiongozi wa juu kabisa wa shirikisho ambalo lilifanya mabadiliko hayo ya katiba kiholela.
Aidha, Wambura alimtaka Tenga
kuwaomba radhi Watanzania kutokana na matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi
wa shirikisho hilo, hali iliyosababisha serikali kuamua kuingilia.
“Tukienda kinyume na uamuzi wa serikali itakuwa ni utovu mkubwa wa
nidhamu, nawasihi wajipime kuhusiana na
kujadili kuhusiana na uamuzi wa serikali kuifuta katiba mpya iliyokiuka sheria.
Badala yake wafanye utekelezaji mara moja.
“Najua watafanya hivyo ikizingatiwa kati ya wajumbe wa kamati hiyo ni
watumishi wa serikali,” alisema wambura.
Serikali iliingilia kati na kuifuta katiba mpya ya TFF iliyopitishwa kwa
njia ya waraka, kitu ambacho kimeonekana ni ukiukwaji wa katiba ya TFF.
TFF ilisema iliamua kutumia waraka kupitisha marekebisho ya katiba kwa
kuwa hawakuwa na fedha za kuitisha mkutano mkuu, kitu ambacho mwisho
kimeonekana si sahihi.
Katiba hiyo mpya, tayari ilitumika kuwapiga panga baadhi ya wagombea
akiwemo Jamal Malinzi aliyekuwa anawania nafasi ya Urais, akichuana na Athumani
Nyamlani ambaye mwisho alibaki kuwa mgombea pekee.
0 COMMENTS:
Post a Comment