March 3, 2013



MWANARIADHA wa Kitanzania, Sarah Ramadhani, jana aliibuka shujaa katika mashindano ya mwaka huu ya mbio ndefu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya kilomita 21, (nusu marathon), kwa upande wa wanawake katika mbio zilizofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.


Wakati Sarah anang’ara, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen raia wa Denmark alikuwa kati ya watu walioshiriki mbio hizo ambazo hugawanywa kwa makundi.
 Sarah alishinda mbio hizo baada ya kukimbia kwa dakika 1:13:05 na kujipatia medali ya dhahabu baada ya kuwabwaga wenzake wakiwemo Wakenya ambao wamekuwa wakitawala mbio hizo katika miaka ya hivi karibuni.

 Katika mbio hizo ambazo mwaka huu zimeweka rekodi ya kuwa na washiriki zaidi ya 6,800, Vicoty Chepkemoi, kutoka Kenya alishika nafasi ya pili baada ya kukimbia kwa dakika 1:14:34, ambapo Mtanzania mwingine Failuna Matanga, alishika nafasi ya tatu kwa kukimbia kwa dakika 1:15:35.

Hata hivyo wakenya waliendeleza ubabe wao, baada ya wanariadha wake kushika nafasi ya kwanza katika mbio za kilomita 42 na kilomita 21 wanaume, pamoja na nafasi ya kwanza katika kilomita 42 upande wa wanawake.

Katika mbio za kilomita 42 wanaume, Kipsang Kipkemoi alishika nafasi ya kwanza kwa kukimbia dakika 2:14:56 na kufuatiwa na mkenya mwenzake Julius Kilimo, aliekimbia kwa dakika kwa dakika 2:15:44 ambapo mkenya mwingine Dominic Kiangor alishika nafasi ya tatu kwa kukimbia dakika 2:16:25.


Kwa upande wa wanawake, mkenya Edna Joseph, alishinda mbio hizo pale alipomaliza kwa dakika 2:39:05 na kufuatiwa na Eunice Muchiri, (Kenya), aliekimbia kwa dakika 2:41:00 na watatu alikuwa ni Fridar Too, aliekimbia kwa dakika 2:44:04.

Akiongea muda mfupi baada ya kuwazawadia washindi, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara, aliahidi ushirikiano wa serikali katika kuendeleza michezo hapa nchini.

 “Nichukue nafasi hii kuwapongeza wadhamini wa mbio hizi, Kilimanjaro Premium Lager pamoja na wadhamini shirikishi mbalimbali wa mashindano haya wakiongozwa na mdhamini mkuu, kwani mbali na kuibua na kukuza vipaji vipya, mashindano haya yametokea kuwa mchango mkubwa katika kuitangaza Tanzania na kukuza uchumi wa Kilimanjaro na nchi kwa ujumla kutokana na kushirikisha watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi”, alisema.

Aliwataja wadhamini wengine kuwa ni pamoja na Vodacom Tanzania, GAPCO, Tanga Cement, CFAO Motors, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, Tanzanite One, New Arusha Hotel, UNFPA, Fastjet na Kilimanjaro Water.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic