NILIKUTANA na shabiki mmoja wa soka, hakutaka kunieleza
anashabikia timu ipi ya soka hapa nyumbani zaidi ya kusema yeye ni Arsenal damu
pamoja na kwamba kikosi cha Arsene Wenger kimekuwa hakieleweki, leo raha, siku
mbili zinazofuata ni karaha tu.
Pamoja na kuzungumza naye mambo yote, muungwana huyo mpenda
soka aliniuliza kama sina hofu na bastola inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Simba,
Ismail Aden Rage ambaye nimekuwa nikimkosoa mara kadhaa kuhusiana na uongozi
wake.
Nilipomuuliza amejuaje kama Rage anamiliki kifaa hicho,
akanikumbusha ile kesi ya ubunge baada ya Rage kupanda na ‘cha moto’ jukwaani,
hali iliyosababisha matatizo kwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Kweli nikakumbuka.
Lakini kwa kuwa si mtu wa siasa, nikamueleza tuachane nayo na
kumsisitizia: “Bastola yake haituhusu, wala haiwezi kunipa hofu ya kusema
ninachoona ni bora kwa soka ya Tanzania, ukweli ndiyo kila kitu.”
Leo nimerudi tena, naendelea na nilichokianza miezi kibao iliyopita
kuhusiana uendeshaji wa Rage, najua wengi wamekuwa wakiniona mkorofi, lakini
naamini kama ni gari, limeshakata breki kwa kuwa nina kila sababu ya kufanya
hivyo.
Rage ameshindwa kuongoza, inaonekana wazi leo. inawezekana
hata mliokuwa mkiniona ninamsakama tu labda kwa sababu zangu binafsi, mnaanza
kuelewa. Naamini mtanielewa zaidi kadiri siku zinavyosonga, kikubwa tuombe
uzima.
Nani asiyejua Simba ilikuwa katika mwendo mzuri sana? Lakini
kila kitu kinakwenda mrama na aibu ndiyo imekuwa zawadi ya Simba kila jua
linapochomoza.
Ushirikiano:
Chini ya uongozi wa Rage, hakuna ushirikiano ndani ya klabu
hiyo kuanzia kwa viongozi na wachezaji, wachezaji wenyewe kwa wenyewe na hata
makocha na vijana. Hakika mambo si mazuri, hali inayoashiria moja kwa moja kuwa
mambo yamekushinda na inaonekana hutayaweza tena.
Simba haigombanii chochote bora tena, kila kukicha inawania
nafuu, haina tena uhakika wa kuchukua ubingwa ambao kiaina imewaachia Yanga na
Azam FC. Nafasi ya pili, huenda ikawa tatizo pia kama mwenendo ndiyo huo.
Yanga walikumbana na ‘aibu’ ya kuwa wa tatu, uongozi wako
unaitengeneza msimu huu kwa Simba. Hatari zaidi, Simba inaweza ikadondokea hata
nafasi ya nne kwa kuwa klabu ina kikosi kisichokuwa na ushirikiano, maana yake
hakina sifa ya kuitwa timu na matatizo yote siku ya mwisho yatakuwa ya uongozi wa
juu.
Msimu uliopita, safi kwenu na mlistahili pongezi. Msimu huu
mmeboronga, ingawa Rage unanishangaza, maana bado unaona unastahili pongezi!
Siasa:
Inaonekana wazi Rage umebanwa, kuna mambo mengi yanatokea
ndani ya klabu hiyo bila wewe kujua. Shughuli za kisiasa zinakubana. Wakati
Simba ikiwa inaendelea kuyumba, mzee wangu wewe ulionekana ukigombea bendera na
kijana mbichi wa Chadema. Katika hilo huna makosa, lakini jiulize ulikuwa ni
wakati wa kuiacha Simba?
Kocha:
Hivi karibuni ulisikika ukimuangushia mzigo kocha Milovan
Cirkovic ambaye mlimtimua, mkashindwa kumlipa hadi msaada wa Malkia wa Nyuki
ndiyo ukaokoa jahazi. Pamoja na kusema Mserbia huyo ni tatizo, leo Simba ina
Mfaransa, mambo ndiyo mabaya zaidi.
Katika hali ya kawaida, haingii akilini kama kweli Simba
ilifanya kitu cha msingi mbele ya uongozi wa Rage. Katika hili wanachama na
mashabiki wa Simba wameonyesha kuchukizwa, ndiyo, wana haki kwa kuwa
wanachotaka ni matokeo mazuri.
Kama Milovan aliondoka, alikuwa na matatizo, basi aliyekuja
alitakiwa kuleta matokeo mazuri kuliko yeye. Sasa Simba inadidimia kuelekea
nafasi ya nne, kitu ambacho mwisho wa ligi kinaweza kusababisha aibu kubwa kama
mwenendo ndiyo huo.
Kujiuzulu:
Nani kasema ni dhambi? Nani kasema kufanya hivyo ni aibu
kubwa? Sasa vipi Rage mbona hautaki kuiokoa Simba kama unaipenda kweli? Kuwa muungwana,
jiuzulu. Mambo mengi yanaonekana kukwama kwa kuwa wewe na uongozi wako,
mmeshindwa.
Utapinga vipi hamjashindwa? Timu haifanyi vizuri, madeni
lukuki kupindukia na wachezaji hawajalipwa fedha zao za usajili,
wanacheleweshewa mishahara. Angalia hivi karibuni, basi la Simba lilizuiliwa na
mwenye hoteli, kisa madeni. Hizo zote ni aibu!
Kukimbia:
Sema hautaki kunisikia tu mzee wangu, hivi karibuni ulifanya
kitu kibaya sana. Ulionyesha wazi ulivyo mjanja kutetea maisha yako kuliko
kuungana na vijana wako na kama ni kuzama baharini, basi mzame pamoja.
Unajulikana kuwa unaipenda Simba, wewe unaipenda Simba ipi?
Labda kama ipo nyingine, maana siku inafungwa na Libolo, wewe ukaikimbia na
kuondoka zako. Tena vibaya zaidi ukawakimbia hadi wageni mawaziri na wabunge
uliokuwa umewaalika. Hakika wewe una roho ngumu...eeh!
Najua Kiswahili kina maneno mengi sana, kila mmoja ana ujuzi
wa kuyapanga kivyake mdomoni, wewe ni mwanasiasa, lazima utakuwa fundi. Lakini
mambo mengi yanakubana, yanaonyesha umefeli, sasa umefika wakati maneno yako
hayafanyi kazi tena. Chukua uamuzi wa busara.
Ahadi:
Nilishakuchambulia ahadi kibao ulizowahi kuahidi ambazo
hujatekeleza, moja ni ile ya uwanja ambayo uliwaonyesha Wanasimba mchoro. Hadi
leo imekuwa ni ahadi isiyotekelezeka na wewe umekuwa mkali kweli kuhusiana na
hilo.
Unajua mengi uliyoahidi ambayo hayajatekelezeka, ushauri
wangu ni huo. Simba ‘unaipenda’ , ninaamini hata yenyewe inakupenda. Lakini kupendana
kunaisha, ni sehemu ya maisha. Unaweza kubaki kama mmoja wa wazee wa klabu na
kuendelea kushauri, pumzika ‘mwayego’ Rage.
Ninaamini wanaosema ninakushambulia au kama unafikiri hivyo
basi unakosea sana. Huenda kwa mara nyingine nimekukumbusha kwa upole sana. Unaonyesha
umeshindwa, nafsi yako itakueleza ukweli. Basi unaweza kuonyesha unaipenda
Simba kwa kuwapa nafasi wengine, kung’ang’ania hakutakusaidia lolote, badala
yake utaendelea kuiumiza Simba ‘yako’.
SOURCE: CHAMPIONI NEWSPAPER
0 COMMENTS:
Post a Comment