March 5, 2013





MARA mbili sasa, nimemsikia mtangazaji mmoja wa redio ambaye anajiita mchambuzi akijaribu kuchangia kuhusiana na suala linalogusa hisia za wapenda soka Tanzania, lakini nikagundua hakuwa na mambo mengi ya msingi zaidi ya kushadadia huenda kwa kujazwa maneno ya kuzungumza.
Haraka haraka nilimchukulia mchambuzi huyo kama mwanasesele ambaye hujazwa ufunguo na baada ya hapo anaachiwa na kuanza kucheza. Mara nyingi kazi yake inakuwa ni kufurahisha watoto.

Kimantiki, kazi ya vyombo vya habari si kufurahisha watoto, si kwa ajili ya kufariji watu fulani hasa linapofikia suala makini kama hilo ambalo wananchi wanataka kupata uhakika wa mambo ambayo hakika yanakuwa yanawachanganya.

Tayari kuna mkanganyiko hapa, suala hili limekuwa likiwagawanya Watanzania wapenda soka kuhusiana na namna linavyokwenda. Huu ndiyo wakati mwafaka wa sisi wanahabari kukaa katikati na kulifafanua wapi sahihi, wapi si sahihi na kipi cha kufanya.

 

Lakini kama kuna watu wameishachagua makundi, wanachofanya sasa ni kuishambulia tu TFF kwa ajili ya maslahi ya watu fulani, nafikiri si sahihi. Pia umakini mkubwa unatakiwa ili tuondoke kwenye zile hisia za waandishi wanatumiwa.

Inaonekana kama mmeshikishwa fimbo muwachape wengine bila ya kujua, maana w0asikilizaji wanaamini kila wanayemsikia kwenye redio ni mwandishi, kitu ambacho si sahihi. Naamini hata wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kuwa makini na watu wanaowapa dhamana ili wasiitumie vibaya nafasi hiyo kama hali inavyokwenda.

Waandishi hawapaswi kuwa upande wa wagombe, mfano Jamal Malinzi, Michael Wambura au Athuman Nyamlani. Wanachotakiwa ni kuripoti, pia kama uchambuzi basi uwe na mashiko, ilimradi umesikika tu redioni, si sahihi.
Kinachoonekana sasa, tokea serikali imetangaza kutoitambua katiba mpya ya TFF na kuendelea kuitambua ile ya mwaka 2006, inaonekana kuna kundi la wale wanaotaka fulani aingie na fulani asiingie, hivyo nguvu imekuwa nyingi katika kampeni badala ya hali halisi.

Wananchi wanataka kujua si kupotoshwa au si huu si wakati wa kupiga kampeni. Mimi niwakumbushe wadau, serikali haiongozwi na malaika, huenda hata uamuzi uliotolewa na waziri pia unaweza kuwa na walakini.
Kikubwa ambacho kinatakiwa kufuatwa ni kuhakikisha serikali na TFF wanakaa pamoja na kulijadili suala hilo ili kuwe na haki ambayo itafuata taratibu na si kutoka nje ya sheria kwa ajili ya kuwanufaisha fulani.

Mimi naunga mkono hivi, hata kama Malinzi pia anaonekana alitakiwa kuondoka kwa kufuata sheria, kama ni haki, basi aondolewe na migogoro isiwepo wala kampeni za kulazimisha zisipewe nafasi. Sidhani kama yeye ndiye anaweza kuwa kila kitu, kwamba akiingia basi soka ya Tanzania itabadilisha kila kitu.
Lakini kama kanuni zitaonyesha Malinzi anastahili kubaki kwa mujibu wa sheria, basi apewe haki yake ya kugombea na mwisho wapiga kura ndiyo watakaokuwa na nafasi ya kuamua nani atakuwa Rais wa TFF.

Nasisitiza, tusikiuke kanuni kwa ajili ya kumuonea au kumpendelea mtu fulani, sidhani kama itakuwa sahihi leo Tanzania iingie katika mgogoro na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa ajili ya kumbeba fulani.
Lakini pia hakutakuwa na sababu ya kuingia katika mgogoro na Fifa kama itaonekana sheria zinakiukwa na kuna mgombea anaondolewa kwa kuonewa kwa mabavu. 

Ninamaanisha, Watanzania lazima tuangalie haki yetu lakini bila ya kuitambuka sheria.
Mwisho maslahi ya taifa letu ndiyo yanakuwa ni ya msingi zaidi, mnaotumiwa katika kipindi hiki pia mnapaswa kuwa makini. Vizuri mnayozungumza mkachimba kwanza kuliko kugeuka wanasesele mnaosema bila ya kuwa na uhakika au ‘pointi’ za kutosha kuhusiana na mnachosema.

Soka ya fitina kupitiliza na mipango ya maendeleo kidogo tuliondoka tokea enzi za Fat, sasa kama kuna wageni hamkuwahi kupita huko, chonde chonde, uoneeni huruma mpira wetu. Hatutaki kurudi huko, jitahidini mtafakari ili muondoke kwenye umwanasesele.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic