March 2, 2013



Mechi ya kwanza iliyowakutanisha Barcelona na Real Madrid ilikuwa ni mwaka 1902 na ilionekana ni kama utani.
Leo mambo ni tofauti kabisa, kwani mechi hiyo inayowakutanisha wapinzani hao wakubwa wa Hispania iliyopewa jina la El Classico imewahi kuangaliwa na watu wapatao milioni 500 kwa wakati mmoja hadi kufikia kupewa jina la “Mechi ya Karne”.

Bado El Classico inaendelea kushika chati ya kuwa mechi maarufu ya watani wa jadi na mechi maarufu zaidi kuliko zote duniani.
Mchezaji bora wa dunia, Lionel Messi wa Barcelona na mshindani wake mkubwa, Cristiano Ronaldo wanaisogeza mechi hiyo kuwa maarufu zaidi na leo huenda mechi hiyo ikavunja rekodi ya kuangaliwa na watu wengi zaidi.


Hali hiyo inatokana na kwamba, mechi itaonyesha muda mzuri ambao wengi wataweza kuiona katika nchi mbalimbali duniani.
Kwa kuwa Tanzania itaonekana saa 12, wengi watapata nafasi ya kuishuhudia kwa kuwa wanalazimika kwenda kuangalia mechi katika hoteli au baa, hivyo inapoonyesha kuanzia saa 5 usiku inakuwa vigumu kwao.

Lakini si Tanzania tu, nchi nyingi ambazo zilikuwa zinaathirika na muda wa kuonyeshwa moja kwa moja kwa mechi hiyo, leo zitakuwa katika nafuu kubwa.
Mechi iliyopita pia itachangia wengi kuangalia mechi ya leo kwa kuwa Madrid iliitandika Barcelona kwa mabao 3-1 na kushangaza wengi, huenda leo Barcelona ikalipa kisasi au vijana wa Jose Mourinho wakaendeleza ubabe. Wengi wanataka kuona kuhusiana na hilo.

Mechi ya leo itakuwa mechi ya tatu Santiago Bernabeu kujaza watu bila ya kubakiza hata nafasi moja baada ya ile ya kwanza ya Nusu Fainali ya Copa De Rey, pia mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Man United.
Mashabiki wengi duniani kote wataweza kuiona mechi hiyo kwa kuwa itachezwa jioni badala ya ilivyokuwa imezoeleka kuchezwa usiku.

Kwa kuwa inachezwa saa 10 jioni, mashabiki wa Tanzania wataiona saa 12 jioni, lakini hata Beijing, China kwenye soko kubwa la timu hizo wataiona mechi hiyo saa 5 usiku badala ya saa 10 alfajiri, hali iliyokuwa inawalazimu kuamka.

Mambo yatakuwa mazuri zaidi kwa mashabiki wa Amerika Kusini na hasa miji yenye wendawazimu wa soka kama Buenos Aires, Argentina na Sao Paulo, Brazil ambao wataiona mechi hiyo saa nne asubuhi. Imeelezwa maeneo mengi ya miji hiyo, kazi na biashara zitasimama wakati wa mechi hiyo.
Nchi nyingi za Uarabuni ambako pia kuna soko kubwa la mauzo ya vifaa vya timu hizo mbili, wataiangalia mechi hiyo saa 12 jioni kama ilivyo kwa Tanzania, hali ambayo inaonekana ni mapinduzi makubwa ya muda tofauti na ilivyozoeleka awali.




DONDOO:

ZILIVYOKUTANA EL CLASSICO:
TIMU                SHINDA         MABAO YA KUFUNGA
Madrid                   89                         376                             
Barcelona              105                       360 
*Jumla zimekutana mara 225 lakini mechi 223 ndiyo za mashindano.

MCHEZAJI ALIYECHEZA MECHI NYINGI:
Manuel Sanchis (Madrid) amecheza mechi 43
Xavi Harnandez (Barcelona), amecheza mechi 37

MCHEZAJI MWENYE MABAO MENGI:
Alfred di Stefano (Madrid) 18
Lionel Messi (Barcelona)  17
Raul (Madrid)  15

MECHI ZENYE MABAO MENGI:
Ukiachana na vikosi hivi vya sasa, tunaangalia mechi za miaka ya nyuma 
za El Classico zilizokuwa na mabao mengi.

Aprili 18, 1926      Barceloba 5... Madrid 1
Februari 3, 1935  Madrid  8...Barcelona 2
Februari 21, 1935  Barcelona 5...Madrid 0
Juni 13, 1943  Madrid 11...Barcelona 1
Mei 19, 1957  Barcelona 6...Madrid 1







0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic