Nimesikia uongozi
wa Simba kuwa unataka upongezwe kutokana na masuala ya kadhaa, moja wapo ni
kumuuza kiungo wake mshambuliaji, Emmanuel Okwi raia wa Uganda kwa klabu ya
Etoile du Sahel ya Tunisia.
Uongozi huo
wa Simba ambao unachukia sana kukosolewa, umeeleza mambo kadhaa uliyoyafanya
kama kupandisha kipato cha Simba lakini pia ‘kumuuza’ Okwi kwa kitita cha dola
300,000 (zaidi ya Sh milioni 450).
Fedha ni
nyingi na kama ingekuwa ni suala la maandishi ya kwenye makaratasi pekee
yanaweza kuonekana ni fedha halisi, basi hilo lingewezekana. Lakini ukweli
walichokifanya Simba ni kitu cha kushangaza.
Kama
watakuwa wanahitaji pongezi, basi wanalazimika kusubiri hadi malipo ya fedha
zote za mauzo yatakapoingia katika akaunti yao. La sivyo wanastahili lawama kwa
kuwa watu wasio makini na wenye kukurupuka kwa kuwa biashara ya Okwi ni
biashara kichaa.
Nasema
biashara kichaa kwa kuwa Simba imeharakisha kumuuza Okwi kama vile ilikuwa na
mipango madhubuti, inaonekana faida ya fedha imekwenda kwa mchezaji mwenyewe au
na mtu mwingine yoyote ambaye huenda ‘amepozwa’.
Lakini
klabu kama Simba, haijafaidika jambo lolote hadi sasa zaidi ya kuendelea
kuathirika katika mambo kadhaa ya msingi, mojawapo likiwa ni kumkosa mchezaji
huyo katika mechi nyingi za ligi.
Angalia
Simba katika kipindi hiki inavyosota katika kila njia, haina fedha, wachezaji
wake wamekuwa wakilipwa kwa mafungu na mambo si mazuri ingawa uongozi umekuwa
ukijitahidi kuficha mambo kwa kuyafunika kwa kisingizio eti unasakamwa.
Leo uongozi
huo unataka upongezwe kwa madudu lukuki uliyofanya, uongozi unajisifia hata
katika suala la Okwi ambalo dhahiri linaonekana ni kama kichekesho kwa kuwa
Simba imefanya biashara ya hisia bila ya kuingiza chochote.
Siku chache
kabla ya kumuuza Okwi ‘bure’, Simba ilikuwa imengia mkataba na mchezaji huo na
kumwaga zaidi ya Sh milioni 40. Halafu yenyewe ikaamua kwenda kumuacha Tunisia
bila ya kupata fedha hata chembe zaidi ya ahadi. Hii ni aina gani ya biashara?
Lakini kama
haitoshi, Simba inataka isifiwe kwa kuongeza kipato cha klabu hiyo, lakini aibu
za timu kuingia katika madeni makubwa yanayopelekea aibu zimekuwa zikizidi.
Basi la
Simba kuzuiwa Arusha kutokana na deni la Sh milioni 15, kuna kiongozi anapinga
hata bila ya haya, lakini hiyo ndiyo hali halisi. Achana na hivyo, wachezaji wa
Simba kuzuiwa dakika chache katika hoteli kabla ya kwenda uwanjani kuivaa
Coastal Union.
Sasa kipato
kama kimekua na sasa Simba inaingiza fedha nyingi ukilinganisha na ilivyokuwa
kabla ya kuingia uongozi wa sasa, kwa nini madudu kama hayo hayaishi? Lakini
uongozi wala hauoni, unataka pongezi!
Uongozi
unajua kama umeshindwa kuingoza timu yake katika mwenendo mzuri, ndiyo maana
mambo mengi sana yamevurugika.
Benchi la
ufundi, wachezaji wakongwe ni matatizo matupu na leo wako wachezaji wanaolipwa
mamilioni ya fedha, hawana faida na timu.
Nasema
hawana faida kwa kuwa hawachezi na sababu za msingi kuwazuia wasicheze hazipo,
ukiulizwa utaambiwa fulani alimuudhi kocha! Wao ni binadamu, maudhi
hayakosekani, yakitokea lakini kuna njia ya maana kuyashughulikia na kikubwa ni
wao kuitumikia Simba.
Lakini
haifanyiki na uongozi kwa kuwa si imara unashindwa kulishughulikia suala hilo,
mwisho inatumika short cut ambayo ni kuwafungia halafu inabaki kwa Simba kwa
kuwa inaendelea kutoa mshahara wa bure wakati mchezaji hapotezi chochote.
Mwisho wa
msimu mchezaji ataondoka zake na kujiunga na timu nyingine, Simba itakuwa
imemaliza msimu kwa aibu. Ukiangalia, hesabu bora zingekuwa ni kufanya mazungumzo
ya pamoja kwanza ili kukubaliana kuhusiana na tofauti zilizopo.
Baada ya
hapo wachezaji hao wangecheza kwa moyo mmoja na kuisaidia klabu, mwisho wa
msimu bado uongozi ungeweza kuwaita na kujadili upya masuala kadhaa na kujua
kama inaweza kuendelea nao au la.
Lakini uongozi
wa Simba, hauna ‘akili’ hiyo ambayo zaidi inalenga kuisaidia timu na pia
kuwasaidia wachezaji kung’amua matatizo yao. Mwisho uongozi unalazimika kulaumu
kwa kuwa unakosolewa.
Unashindwa kuwa
na hoja za msingi kwa kuwa unaona umeharibu na kukubali kwamba wenyewe ni
chanzo ni kama ‘dhambi’ kubwa.
Haya ni
machache, yako mengi ambayo uongozi unapaswa kuangalia kwa maana ya kujifunza,
kujirekebisha na ikiwezekana kukubali kukosolewa. Cha kuwapongeza kinaweza
kuonekana kwa darubini kwa kuwa kinafichwa na madudu lukuki. Najua mme-miss
kupongezwa, haya basi Hongera uongozi wa Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment