April 8, 2013


Simon Msuva na Frank Domayo wa Yanga na Taifa Stars baada ya mazoezi ya Yanga..


*Wako wanaopanda mishikaki kwenye bodaboda

Na Saleh Ally
TAKRIBANI wiki nne nilikuwa kwenye mazoezi ya asubuhi, ilikuwa kwenye Viwanja vya Leders, nikashuhudia kitu ambacho kilinishangaza kiasi fulani.

Siku chache baadaye, nilikuwa katika mazoezi ya Yanga kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama jijni Dar, nikaona kitu kama nilichokiona katika mazoezi ya Simba, nitakueleza.

Kila baada ya mazoezi ya timu hizo mbili kubwa kumalizika kunakuwa na usafiri wa basi ambao unatolewa na uongozi kwa ajili ya wachezaji hao. Lakini kawaida wengi hawapendi kupanda pamoja katika basi hilo.

Rashid Mkoko wa Simba baada ya mazoezi..

Wengi wanachumua usafiri binafsi, ukianza na wale wenye usafiri wao binafsi na baada ya hapo wale wanaokodi Taxi, Bajaj au Bodaboda kurejea makwao. Si kitu kibaya, lakini kuna maswali kadhaa nikaanza kujiuliza.

Maswali yangu yalianza baada ya kuona wachezaji wa Simba wanapanda Bajaj na wale wa Yanga pia, ingawa Simon Msuva na Frank Domayo ndiyo walinishitua zaidi baada ya kupanda pikipiki moja maarufu kama ‘mshikaki’. Siku chache nilimuona Rashid Ismail Mkoko akipanda Bajaj. 

Yaani Domayo na Msuva wa Yanga, wamepanda mshikaki! Acha tu kwamba ni wachezaji wa Yanga, lakini ni wachezaji wa kikosi cha timu ya taifa , Taifa Stars!

Sitaki nionekane ninadharau usafiri wa Bodaboda na Bajaj, lakini najaribu kuonyesha kiasi gani uongozi wa klabu hizo mbili unavyoweza kufanya na kubadilisha mambo. Hakuna ubishi kupanda mshikaki katika Bajaji ni kuvunja sheria, lakini ni hatari sana kwa afya ya wahusika.

Msuva na Domayo leo ni tegemeo la Wanayanga ambao wako zaidi ya milioni 10 nchini, lakini pia ni tegemeo kwa taifa letu lenye watu zaidi ya milioni 40. Sasa vipi wapande kwenye pikipiki, tena mshikaki!

Sitaki kuwafananisha wachezaji hao wa Yanga na Simba sawa na wale wa Man United kama Wayne Rooney, Cristiano Ronaldo (Real Madrid) na wengine. Lakini kuna sehemu inafikia, mchezaji anatakiwa kuwa na usafiri wake binafsi.

Pele aliwahi kusema, gari lake aina ya Mercedes Benz ambalo alihofia kulinunua, liligeuka na kuwa changamoto ya kumshawishi acheze vizuri kwa kuwa alihofia akiharibu, basi atalazimika kuliuza, ila akijituma, atapata fedha za kununua gari bora zaidi ya alilokuwa nalo.

Ninaamini inawezekana kabisa mambo yakaenda tena vizuri bila ya wachezaji hao kupanda mshikaji kwenye pikipiki na ubunifu ukifanyika unaweza kubadili hali hiyo.

Klabu:
Klabu nyingi za Ulaya zimeingia mkataba wa kuyatangaza makampuni ya magari ambayo pamoja na mamilioni ya fedha zinazotoa kama watangazaji, lakini zinatoa magari kwa wachezaji wa timu hizo kwa bei nzuri yenye unafuu mkubwa.

Mfano mzuri ni Real Madrid na Man United zinazotangaza magari ya Audi, Arsenal na Citroen na Liverpool na Chevrolet.

Hapa inawezekana, hata kama kwa makampuni yanayouza magari yaliyotumika yakajitangaza na Yanga au Simba na mwisho nayo yakatoa punguzo kubwa kwa wachezaji watakaotaka magari. Hapa siku ya mwisho, klabu, watangazaji na wachezaji, wote wanafaidika.

Wachezaji:
Hadi kufikia kucheza katika klabu kubwa au timu ya taifa, gari haiwezi kuwa starehe tena. Ni wajibu kwa kuwa kuna mambo kadhaa mchezaji anatakiwa kuyafanya.

Mfano, baada ya mazoezi, anatakiwa kuingia kwenye gari lake na kwenda nyumbani kupumzika. Lakini si kugombea daladala, au kuhangaika kuuma meno akiwa amemkumbatia dereva wa bodaboda.

Mara nyingi wanafanya mazoezi mara mbili kwa siku, jiulize safari ya kwenda na baadaye kurudi tena mazoezini kwa kugombea usafiri wa jamii. Nafikiri inabidi mlifanyie kazi hilo na inawezekana tu.

Gari si ufahari tena, inawezekana mkanunua za bei nafuu kwa ajili ya kusaidia utendaji wenu lakini kuendana na mlipofikia.

SOURCE: CHAMPIONI NEWSPAPER

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic