Unaweza kufikiri nimeshindwa kuwa mvumilivu au
ninachokizungumzia huenda nimekikatia tamaa. Hilo sahau na halitatokea, labda
mninyamazishe milele. Kwanza nianze na salamu za sikukuu ya Pasaka kwa wote
mlioisherehekea.
Nimeanza na kuzungumzia kukata tamaa kwa kuwa
nimejaribu kutafakari namna mambo yanavyokwenda katika mchezo wa soka. Ninaamini kila kitu ni afadhali ya jana.
Nasema afadhali ya jana kwa kuwa sioni kama tunapiga
hatua. Angalau kidogo katika timu ya
taifa kumekuwa na mabadiliko ambayo yanatia moyo lakini bado nitaumia sana kama
tukishindwa kufuzu kwa kuwa hakutakuwa na tofauti sana.
Angalau tofauti nyingine ni Azam FC, timu ambayo hadi
sasa ndiyo wamebaki wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa.
Wale wakongwe ambao ukubwa wao ni majina, hakuna anayeendelea kuliwakilisha
taifa.
Stars na Azam FC ndiyo matumaini makubwa, Simba na
Yanga ambao ni wakongwe bado hawako katika nafasi nzuri hata kiuchezaji, ndiyo
maana umesikia hadi uongozi wa timu hizo unalalama.
Ndani ya miaka sita au zaidi, timu hizo mbili au timu
nyingine yoyote ya soka ya Tanzania haiwezi kusema ilikuwa na mafanikio katika
michuano ya kimataifa.
Yanga wanaweza kujivunia michuano ya Kombe la Kagame. Hii
ni michuano ya kanda, angalia ile iliyo chini ya Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa) au Shirikisho la Soka la Afrika (Caf), timu hizo hazina
nafasi.
Kama miaka inakwenda, hata kama kweli tunasema timu
zetu zinajifunza, vipi hakuna mabadiliko wala mafanikio? Umri wa wahusika unapiga hatua, mabadiliko
hakuna na mambo yako palepale.
Unaweza kumgusa kila mtu kati ya waliopita na kupewa
nafasi ya uongozi. Wako waliokuwa wakongwe
katika michezo kwa maana kwamba walikuwa wachezaji, ambao hawakucheza lakini walikuwa
wasomi.
Lakini bado mafanikio hayakuwepo, badala yake migogoro
imekuwa ikiendelea kuchukua nafasi hata watu wanapobadilika au wale wanaoonekana
wanaweza, wakipewa tu nafasi ya uongozi nao wanakuwa tatizo.
Lakini wengi pia wamekuwa ni watu wanaoangalia nafsi
zao badala ya maendeleo ya michezo. Tujiulize
mwisho wetu ni nini? Na kama soka ni
mchezo tunaoupenda, vipi tunataka kuwa nao karibu bila ya kuusaidia upige
hatua?
Unachokipenda lakini hutaki kipate mafanikio! Wapo viongozi wameamua kurejea shule na kusoma
ili waje waongoze soka. Hilo si jambo baya. Lakini hadi leo wanashiriki katika
migogoro ya mchezo huo kila kukicha na wao ndiyo vinara.
Watu wanachaguana au kupeana sapoti kwa kufuata
ukabila au udini. Fedha zinawatoa watu roho, hawajali kwamba mchezo wa soka
unasukumiwa viongozi wasio na uwezo. Wanajua
kabisa lakini njaa inakuwa muongozo kwao.
Wakati mwingine najiuliza, kama ingekuwa inawezekana
labda kizazi chetu, yaani cha wakati huu, kingepotea ili mchezo wa soka na
mingine ipate msaada.
Au tukubaliane, wale viongozi wa zamani aina ya kina Ismail Aden Rage wasipewe nafasi tena
kwa kuwa tumewaona na hawajatusaidia kitu.
Bado ninaamini mapenzi ya dhati yanaweza kubadilisha
mambo mengi sana. Kama watu wataumia, yaani
wakaumia na kutaka maendeleo ya timu zao na mwisho mchezo wenyewe wa soka, basi
hakika tunaweza kubadilika.
Mabadiliko kwenda kwenye mafanikio yanatakiwa kuanzia kwa
mtu mmojammoja, tusikubali kuwa wanasesere, tusikubali kutumiwa tu au kuutumia
mchezo wa soka kujinufaisha. Tuusaidie na ikiwezekana wanaousaliti wawe
wachache ili usonge mbele.
Kwa sasa wanaousaliti mchezo wa soka wako wengi zaidi
ya wanaoupenda na kuuunga mkono. Mbaya
zaidi, wasaliti wengi wamepata nafasi za uongozi. Hivyo wanaua soka kwa urahisi
zaidi. sikieni maumivu waungwana, kubalini kuwa
maendeleo yanaweza kupatikana kama nyie mlio na nafasi mkikubali yapatikane.
0 COMMENTS:
Post a Comment