Na Saleh
Ally
KUNA mambo
mengi yamepita katika historia ya soka ya Tanzania, lakini kuna baadhi ambayo
kamwe ni vigumu kuyasahau na huenda yakabaki kuwa gumzo kwa kipindi kirefu
sana.
Mabao
mawili, moja kila mechi aliyoyafunga mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Said Sued
‘Scud’ mwaka 1991 wakati timu yake ikiibuna na ushindi wa mabao 1-0 kila mechi,
gumzo lake halitaisha.
Scud
alikuwa gumzo wakati huo kutokana na uwezo wake wa kupachika mabao, uwanjani
hakuwa mchezaji mwenye mambo mengi lakini alichojua ni ‘kucheka’ na nyavu.
Said Sued 'Scud' wa tano kulia kiwa na Yanga mwaka 1991 |
Mshambuliaji
huyo wa zamani wa Yanga ameamua kurejea kwao Kigoma, anaishi akiendelea na
maisha ya kawaida, pamoja na kufaya biashara zake amekuwa ni mfugaji.
Katika
mahojiano maalum na Championi Jumatatu, Sued anaelezea mambo yakiwamo wakati
wanacheza, lakini mpira wa sasa pamoja na wachezaji.
“Soka la
enzi zetu lilikuwa na changamoto na ushindani mkubwa, mfano wakati nikiwa Yanga
nilikuwa nagombea namba na watu kama wanne au zaidi, kulikuwa na Sanifu Lazaro
‘Tingisha’, Ramadhani Kilambo, Joseph Machela na John Mngazija.
“Makocha
wetu (Syllersaid) Mziray na (Boniface) Mkwasa walikuwa katika wakati mgumu,
hivyo muda wote tulikuwa katika kuwania namba. Hauwezi kuacha kijituma hata
kidogo,” anasema Scud.
Simba v Yanga:
Mechi hii
huwa ya kawaida kabisa unapokuwa uwanjani, lakini mashabiki wanaifanya inakuwa
kubwa na hofu sana. Mimi sikuwa na uoga hata kidogo, hata zile mechi
nilizowafunga Simba nilijua nitafunga kwa kuwa nilipania kufanya hivyo na
nilikuwa fiti sana.
Beki anayemvutia:
Sikuwa na
uoga kwa mabeki hata kidogo, wakati huo kulikuwa na mabeki wengi sana wazuri na
wenye uwezo mkubwa ukilinganisha na sasa.
Ila
nilivutiwa sana na beki wa Reli Morogoro, Fikiri Magoso ambaye baadaye
alikwenda Simba. Alikuwa anaijua kazi yake, ni kati ya mabeki wenye kiwango cha
juu sana. Nakumbuka pia Simba walikuwa na watu kama Mavumbi Omari, Iddi
Selemani, Twaha Hamidu ‘Noriega’, pia kiungo walikuwa na mtu kama Hamis Gaga, haikuwa
kazi lahisi.
Jina Scud:
Hakika
sijui nani hasa alinitunga, sikuwahi kumuona mtu mmoja akisema yeye alianzisha
jina hili ingawa lilianza katika kipindi ambacho kulikuwa na vita ya Ghuba ya
Uajemi kati ya Iraq iliyokuwa inaongozwa na Saddam Hussein dhidi ya Marekani na
washirika wake.
Sasa
nilikuwa napiga mashuti makali sana, hivyo wakawa wanayafananisha na mabomu ya
Scud. Kuna wakati Simba walisema watanitafutia Patriot (mabomu yaliyokuwa
yanaangusha Scud), lakini hadi nastaafu sikuiona.
Bao kutorudi:
Kweli
nilikuwa nikifunga mabao mengi sana hayarudi, naona kama ilikuwa inatokea
lakini mara nyingi nilikuwa nikisali na kumuomba Mwenyezi Mungu kwanza
anisaidie nifunge na iwapo nitafanikiwe kufanya hivyo basi bao lisirudi.
Lakini pia
nilikuwa nikifanya juhudi za mazoezi na maandalizi ya kutosha kila mechi, nilikuwa
sitaki kucheza bila ya kufunga. Ndiyo maana nashangazwa siku hizi kumuona
fowadi anaingia katika eneo la hatari la kwa zaidi ya mara tatu hajapiga
golini, au mshambuliaji eti anacheza dakika 45 bila ya kupiga shuti golini.
Bao bora:
Wengi
wamekuwa wanayazungumzia mabao niliyofunga dhidi ya Simba, lakini bao bora
ninalolikumbuka sana nakumbuka nilifunga Zanzibar. Tuliweka kambi kujiandaa na
mechi dhidi ya Simba.
Tukawa
tunacheza mechi za kirafiki, nakumbuka ilikuwa mechi dhidi Mlandege, Yanga
tulishinda mabao 2-0, moja lilifungwa na John Alex ‘Rwena’ na mimi nikafunga
moja ambalo nilipiga shuti kutoka katikati ya uwanja.
Kipa
alipiga goal kick, ule mpira wakati unaanguka katikati ya uwanja wakadhani
nitautuliza. Lakini sikufanye hivyo, kabla haujagusa chini, nilipiga shuti la
moja kwa moja, alichofanya kipa ni kugeuka na kuukota nyavuni.
Mechi ngumu:
Sijawahi
kucheza na Simba mechi ikawa ngumu sana hadi nikachanganyikiwa, ila tulikuwa
tukikutana na Pamba ya Mwanza, hata sisi tulikuwa tunaambiana kwamba kuna kazi
kubwa mbele yetu.
Nakumbuka
mwaka 1991 tulipokwenda Kanda ya Ziwa, nilianza nikafunga Shinyanga, tulipokuwa
Kagera nikatoa pasi kwa Abubakari Salum ‘Sure Boy’ akafunga bao la ushindi.
Tukarudi
Mwanza, mechi dhidi ya Pamba haikuwa mchezo kama kawaida. Nilianza kufunga bao
safi sana, lakini wakati tunaona tumeshinda Pamba walipata bao la kusawazisha
nakumbuka mfungaji alikuwa ni Hamza Mponda. Mechi ilimalizika kwa sare ya 1-1.
Kwenda Yanga:
Nilitua
Yanga nikitokea Kurugenzi Kigoma, nilisajili hapa Kigoma. Kawaida Yanga ilikuwa
ina wawakilishi wake ambao wanaangalia wachezaji mikoani.
Wa hapa Kigoma
walikuwepo akina Mzee Kayombo, Kingalu na Arif Sharif ambaye nilipelekwa kwake
Ujiji ambako nikasaini fomu za kuichezea Yanga.
Waliniona
katika michuano ya vijana ya taifa iliyofanyika Tabora, nilifunga bao kila
mechi. Nikaibuka mfungaji bora. Nakumbuka fainali tulicheza na Tabora.
Washambuliaji:
Kila timu
ya Ligi Kuu Bara wakati huo ilikuwa na mshambuliaji hatari sana, hata ukienda
Zanzibar ungekuta hivyo. Kabla hamjakutana na timu kuna wachezaji mnakuwa
mnawazungumzia kutokana na umahiri wao.
Lakini leo
hakuna, hili pia ni tatizo la wachezaji wengi kutokuwa na vipaji na
wanaojituma. Wengi wanaingia katika soka kutokana na kujuana au nafasi za ndugu
au wazazi wao katika soka lakini si uwezo wao hasa.
Hivi
karibuni nilikuwa Dar es Salaam, nikaiona Taifa Stars ikicheza na kuifunga
Cameroon bao 1-0, kweli bado sijaridhishwa na viwango.
Siasa na soka:
Soka
inayumba kwa kuwa watu wengi wanaongoza kutokana na kuwa na fedha, au wana
malengo ya kufanikiwa katika siasa au biashara zao na si kuundeleza mpira.
Hao wakiona
unataka kuongoza basi wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanakutoa,
wanajua hawakucheza, hivyo hawataki uwe karibu. Mimi sipendi kuiudhi nafsi yangu,
ndiyo maana najiweka kando lakini naumia sana kuona mchezo huu unapokwenda.
Scud ni
kati ya washambuliaji waliovuma kwa kipindi kifupi, lakini uwezo wao wa kufunga
tokea akiichezea Coop ya Mwanza ulikuwa ni mkubwa sana.
Anasema
huenda akaamua kufanya kazi ya ukocha kwa kuwa tayari amesoma kozi ya awali na
anategemea kujiendeleza zaidi kimasomo na ikiwezekana afundishe.
0 COMMENTS:
Post a Comment