Klabu ya
Simba ni kati ya zile zilizopoteza kabisa mwelekeo msimu huu, shahidi wa kwanza
katika hili utakuwa ni uongozi wa klabu hiyo.
Nasisitiza
hili, kwamba uongozi wa Simba unapokosolewa hujenga makusudi hisia za kuonewa
au kuhujumiwa, lakini hali halisi iko hivi, uongozi huo unajihujumu wenyewe kwa
kuwa umejaza watu wengi wanaoangalia maslahi yao wenyewe.
Mwenyekiti
wake, Ismail Aden Rage anajua kama amepoteza mwelekeo, lakini amekuwa akilalama
kuhujumiwa na kwa kuwa ni muoga wa kujibu hoja zinazoelekezwa kwake, ndiyo
maana anajenga mazingira ya vitisho na uzio wa kutaka asielezwe, labda si
Metodo, sitaacha kumueleza ukweli na vitisho si kitu cha kunirudisha nyuma.
Simba
imepoteza mwelekeo katika kila kitu, ukianzia kwa uongozi hakuna ushirikiano
wala kuaminiana. Ukirudi katika kikosi chenyewe ndiye kabisa, amani na upendo
vimetoweka na kila mmoja anakwenda njia yake.
Marubani
ambao ni Rage na viongozi wenzake wameishapoteza mwelekeo, hawawezi tena kukirudisha
‘chombo’ katika nia yake sahihi, ndiyo maana hakuna upendo na amani ndani ya
timu na klabu kwa ujumla.
Mwanasimba
yupi anaweza kusema anafuraha katika kipindi hiki, anzia mashabiki, wachezaji
hata benchi lote la ufundi.
Simba
imeamua jambo moja, kwamba badala ya kuwatumia wachezaji wakongwe ambao wanadai
wana matatizo, wamewachukua vijana na kuwapandisha, wameamua kuwaamini ili
wapambane. Ni jambo zuri sana.
Lakini bado
tatizo linaendelea kubaki palepale kutokana na uongozi kutokuwa makini na
kufanya mambo mengi kwa mfumo wa kubabaisha na wanapokosolewa au kukumbushwa wanalia
eti wanahujumiwa, upuuzi!
Vijana
ambao Simba wameamua kuwaamini nao wamekuwa wakilia kuhusiana na maslahi yao,
kwangu naona ni kitu cha ajabu sana kusikia vijana hao wanadai mishahara yao ya
miezi kadhaa na hawajalipwa.
Nashangaa
zaidi kusikia hata mikataba waliyotaka kuwasainisha waliwaomba ‘wawakope’,
kwamba walitoa ahadi ya fedha watakayowapa, halafu baada ya hapo watawalipa
siku nyingine baada ya kusaini! Si kitu kizuri.
Pia si
sahihi kuwaona vijana hao kama wana shida sana, au ni wale wanaoibembeleza
Simba kwa kuwa hawana pa kwenda. Hadi leo wanacheza bila ya kuwa na mikataba na
timu hiyo.
Kuna macho
ya wengi, wanaiona kazi yao. Siku kijana ataamua kuondoka na kufuata suala la
maslahi, halafu uongozi uanze kutangaza ni msaliti kama ilivyokuwa kwa Kelvin
Yondani ambaye alitafutiwa uadui wakati tatizo kubwa lilikuwa kwa uongozi wa
Simba.
Vijana
kweli wanachipukia, lakini wanapaswa kupewa motisha, kulipwa mishahara mizuri
nikiwa na maana wapewe mikataba bora ambayo itawafanya wajitolee zaidi na si
kupewa maneno na ahadi nyingi na yule anayefunguka na kuhoji anaonekana mbaya.
Morali
haipatikani sehemu yenye njaa, wote tunalijua hili. Sasa si sahihi fedha
zinaoingia ndani ya Simba kupitia vyanzo kama wadhamini, fedha za milangoni na
malipo ya pango la majengo ya Simba, kuingia kwenye mifuko ya wachache ambao
wanajidai eti wanaipenda zaidi klabu hiyo, halafu wanaotoka jasho zaidi ndiyo
wanaumia.
Kuwachukulia
vijana kama watoto wa shule ni kosa, ndiyo maana mnawapa nafasi ya ya kupambana
na timu nyingine mkiamini wanaweza kufanya vizuri. Basi walipeni vizuri ili
waifanye kazi yenu katika kiwango cha juu.
Nawakumbusha
vijana hao si ‘maroboti’, wana akili zao timamu na wana malengo yao ndiyo maana
wamefikia walipo. Tambueni wanajua wakifanyacho hivyo fanyeni nao kazi kwa
kufuata utaratibu mkiamini wanajitambua.








0 COMMENTS:
Post a Comment