Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa
Stars) itashiriki michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa
Afrika (Cosafa) itakayofanyika Julai mwaka huu nchini Zambia.
Taifa Stars inashiriki michuano hiyo
ya timu za Taifa za nchi wanachama wa Cosafa ikiwa timu mwalikwa. Nchi
wanachama wa Cosafa ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Comoro, Lesotho,
Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Swaziland, Zambia
na Zimbabwe.
Michuano hiyo itafanyika kuanzia
Julai 6 hadi 21 mwaka huu katika miji ya Lusaka, Ndola na Kabwe. Ratiba ya
makundi ya michuano hiyo itapangwa Mei 3 mwaka huu jijini Lusaka.
Mara ya mwisho michuano hiyo
ilifanyika miaka mitatu iliyopita. Hii itakuwa mara ya pili kwa Tanzania
kushiriki michuano hiyo baada ya kucheza ya kwanza iliyofanyika mwaka 1996
nchini Zimbabwe.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager inatarajia kuingia kambini mwishoni mwa mwezi ujao
kujiandaa kwa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8
mwaka huu jijini Marrakech.
Juni 16 mwaka huu Taifa Stars
itacheza na Ivory Coast jijini Dar es Salaam katika mechi nyingine ya mchujo ya
Kombe la Dunia wakati Juni mwishoni na Julai mwanzoni itacheza mechi ya Kombe
la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) dhidi ya Uganda.
Wakati huo huo, waandishi wa habari
wanaotaka kuripoti michuano hiyo wanatakiwa kuwasilisha majina yao TFF kabla ya
Aprili 27 mwaka huu ili maombi yao yatumwe Cosafa kwa ajili ya kupatiwa
vitambulisho (Accreditation).
.jpg)







0 COMMENTS:
Post a Comment