Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa mipira zaidi ya 1,200 yenye thamani ya
dola 30,000 (Sh milioni 50) kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania
Bara na vituo 21 vilivyo hai vya kuendeleza vijana (academies).
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) lilimpa Rais Tenga fedha hizo ikiwa ni shukrani kwake kwa
kushughulikia mgogoro wa uongozi wa mpira wa miguu nchini Kenya uliodumu kwa
miaka miwili; ambapo nchi hiyo kutokana na mgogoro huo ilikuwa na vyama viwili
(KFF na FKL).
Akizungumza katika hafla ya
kukabidhi mipira hiyo kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Aprili 22 mwaka
huu), Rais Tenga amesema amefanya hivyo kwa vile anaamini kuwa mipira ndiyo
kitu muhimu katika kuinua mchezo huo mahali popote.
“Dhamira yangi si kushukuru kwa
hafla hii, bali kutoa sababu kwa nini nimefanya hivi. Ninaamini kwa kuanzia
mipira ndiyo muhimu, pili kwa kufanya hivi itaonekana kweli mipira imegawiwa,”
amesema Rais Tenga.
Amesema amesema mpira wa miguu kwa
Tanzania unahitaji sana watu wa kujitolea, na yeye amefanya hivyo kwa kujitolea
kutokana na ukweli shughuli anazotumwa na FIFA ni za kujitolea.
Rais Tenga ambaye pia alitumwa na
FIFA kutatua matatizo ya uongozi wa mpira wa miguu katika nchi za Uganda,
Zambia na Sudan Kusini amesema anaamini anapata fursa hizo kutokana na kuwa
kiongozi wa TFF, na kwa kuwakumbuka waliomchagua ndiyo maana hakusita kupeleka
fedha hizo kwenye mipira.
Amesema moja ya ndoto zake wakati
anaingia kuongoza TFF mwaka 2004 ameshindwa kutimiza ni kusaidia mipira, kwani
uwezo wa kununua mipira kwa wanaocheza katika ngazi ya chini hasa watoto haupo.
“Hizi kelele zote za maendeleo ya
mpira wa miguu ni kwa sababu shuleni hakuna vifaa. Nia yangu ilikuwa shule zote
zipate mipira, lakini hiyo ni moja ya ndoto nilizoshindwa kutekeleza. Vipaji
haziwezi kupatikana kama watoto hawachezi.
“Tunashukuru sana kwa Serikali
kurejesha mpira shuleni. Hata nitakapoondoka madarakani nikipata nafasi
nitaendelea kuomba mipira kwa ajili ya shule,” amesema Rais Tenga.
Vyama vya mikoa ambavyo jumla ni 32
(Tanzania Bara na Zanzibar) kila kimoja kimekabidhiwa mipira 25 (kumi saizi
namba tano, 15 saizi namba nne kwa ajili ya vijana). Kwa academies ambazo ni 21
kila moja imepewa mipira 25 (minane saizi namba tano, na 15 saizi namba nne).
Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Almasi
Kasongo, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) Nassib
Mabrouk na Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Riziki
Majala.
Kwa upande wa shule alikuwa Kanali
mstaafu Idd Kipingu ambaye ni mmiliki wa shule ya Lord Baden ya Bagamoyo mkoani
Pwani.








0 COMMENTS:
Post a Comment