Karibu kila
kukicha kumekuwa na vita kubwa inayohusiana na makato ya mapato katika viwanja
vya soka katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Malalamiko
hayo yanatokana na namna timu ambavyo zimekuwa zikikatwa fedha huku wadau
wengine wakifaidika wakati hawatoi fedha nyingi kujiandaa na mchezo kama
inavyokuwa kwa timu.
Vita hiyo imekuwa ikipamba moto ingawa naweza
kusema wadau kadhaa kuanzia katika vyombo vya habari hadi ndani ya klabu
zenyewe wamekuwa ni waoga kupambana zaidi.
Hawasimami
na kuzisaidia klabu, inawezekana ni uoga wa nafsi au kuamini hawana haja ya
kupiga kelele kwa kuwa hawafaidiki. Lakini ndani ya klabu hizo, kukaa kimya kwa
viongozi, huenda wanaona hawana sababu ya kuhangaika kwa kuwa wanapata ‘kitu’
kupitia mlango wa nyuma.
Kelele za
wachache ambao tuliamini tunaweza kusaidia, zilichangia kusaidia serikali
kuamka na kutangaza kupunguza makato kadhaa kama yale ya uwanja ambayo mengi
yalikuwa yanajirudia na kuwafaidisha wengine.
Mimi naanzisha
vita nyingine, lengo ni kusaidia kupatikana kwa mabadiliko angalau kama yale
yaliyotokana na kupunguzwa kwa makato.
Ukiangalia
makato ya kila mchezo wa Ligi Kuu Bara, utaona kuna makato yanayokwenda kwenye
Mfuko wa Maendeleo ya Soka au Football Development Fund (FDF).
FDF
inahusika na maendeleo ya soka, lakini bado sijawahi kusikia kwa mwaka
wameingiza shilingi ngapi na zimetumika namna gani zaidi ya kupata ufafanuzi
kidogo kutoka TFF kwamba fedha hizo zinatumiwa na timu za vijana.
Nimeelezwa
kutoka TFF kwamba fedha hizo wala hazitoshi kwa na shirikisho hilo limekuwa
likilazimika kufanya juhudi kutafuta kwingine ili kuzisaidia timu hizo. Kweli
hilo linawezekana, nakubaliana nao.
Lakini hofu
yangu ni moja, TFF inachukua fedha hizo na mimi narudi kwenye hoja yangu ya
kwanza ya mapato nilioyoianzisha. Kwamba inachukua fedha zaidi ya mara moja,
yaani inachukua asilimia kadhaa za mapato kama shirikisho na baadaye kupitia
FDF.
Lakini kitu
cha ajabu, sijawahi kusikia fedha za FDF zikitajwa kwamba zilitumika hivi au
vile, au zilisaidia kiasi gani. Imekuwa kimya tu na fedha hizo za makato kwenda
FDF zimekuwa kama vile mto unaoingia baharini.
Lazima
tukubaliane, fedha hizo ni za umma. TFF wanapaswa kuwa wazi na kutueleza
zinatumikaje, zimekupungua kiasi gani na wanahitaji nyongeza ya kiasi gani
huenda ikawasaidia hata wadhamini kujua kama wanahitaji nini.
Haiwezekani
fedha zinazotokana na makato ya mapato ya klabu tuambiwe zimeingia kuendeleza
soka, lakini hatujui zinaendeleza soka vipi zaidi ya kusikia juujuu tu, eti
hutumika katika timu za vijana.
Mara
kadhaa, nilitafuta kutaka kujua anaouendesha mfuko huo, nilidhani serikali.
Lakini kama ni TFF, ukimya wao kutouzungumzia mfuko huo hata siku moja Napata
hisia za ufujaji na kuna kila sababu ya wao kuwa wazi na kutueleza.
Fedha hizo
zinakatwa hadharani, kwenye taarifa zake kwa vyombo vya habari TFF inaelezea
makato hayo. Ndiyo maana naona nna haki ya kuhoji, matumizi yake ni vipi lakini
angalau msimu huu waliingiza kiasi fani katika mfuko huo.
Mara kadhaa
nimesikia TFF ikisema wana upungufu katika fedha kwa ajili ya kuzihudumia timu
za vijana. Huwa ni Sh ngapi na fedha za FDF huchangia kwa kiasi gani?
Klabu na
viongozi wake zimekaa kimya, hazitaki kuhoji wala hazina haja ya kujua kama
ilivyo kawaida yao, lakini ninaamini wako wenye kiu ya kutaka kujua kama ilivyo
kwangu. Hivyo TFF lazima ijue fedha hizo ni za umma na wadau wana haki ya
kujua, basi watueleze.
0 COMMENTS:
Post a Comment