Taifa
Stars imetua jijini Addis Ababa, Ethiopia leo (Mei 28 mwaka huu) alfajiri kwa
ndege ya EgyptAir ambapo itaweka kambi ya wiki moja kujiandaa kwa mechi ya
mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco (Lions of the Atlas) itakayochezwa
Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.
Stars
iliyotua na kikosi cha wachezaji 21 imefikia hoteli ya Hilton, na imeanza
mazoezi leo (Mei 28 mwaka huu) saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Addis.
Kwa
mujibu wa Kocha Kim Poulsen, Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
itakuwa na vipindi (sessions) vinne vya mazoezi kabla ya kucheza mechi ya
kirafiki na Sudan (Nile Crocodile). Mechi dhidi yan Sudan itachezwa Jumapili
kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Addis.
Sudan
ambayo pia imeweka kambi yake Addis Ababa kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya
Kombe la Dunia ilicheza mechi yake ya kwanza jana (Mei 27 mwaka huu) dhidi ya
wenyeji Ethiopia na kulala mabao 2-0.
Wachezaji
wanaounda Stars ni nahodha Juma Kaseja, nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini
Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir,
Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum
Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd,
Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.
Kikosi
hicho kinatarajiwa kuondoka Addis Ababa kwenda Marrakech alfajiri ya Juni 3
mwaka huu kwa ndege ya EgyptAir. Stars itatua siku hiyo hiyo Casabalanca na
kuunganisha moja kwa moja kwenda Marrakech.
0 COMMENTS:
Post a Comment