![]() |
| MASATU (WA PILI KULIA WALIOSIMAMA) WAKATI AKIICHEZEA PMSSB YA INDONESIA |
Na Saleh
Ally
Kati ya
mabeki waliowahi kucheza soka nchini na majina yao hayapotea midomoni mwa
mashabiki wa soka ni George Magere Masatu.
Masatu
alikuwa na sifa nyingi sana, lakini utambulisho wake lilikuwa ni umbo lake dogo
lakini uwezo mkubwa ulifunika kila kitu na kupingana na mfumo wa soka unaoagiza
beki wa kati lazima awe na umbo kubwa ili kucheza vizuri.
Masatu
alianza kupata jina kubwa wakati akiwa katika kikosi cha Pamba ya Mwanza
kilichotikisa soka nchini, lakini baadaye akaendeleza makali yake akiwa na Simba.
Baada ya
kucheza soka nchini baadaye Uarabuni, Masatu aliondoka nchini na kwenda
Indonesia ambako alicheza soka kwa zaidi ya miaka mitano kabla ya kustaafu na
baadaye akapata kazi katika shule ya watoto iliyo chini ya klabu maarufu ya
England ya Arsenal ambako alifanya kazi kwa miaka mitatu na ushee.
Masatu
anasema sasa amerejea nyumbani Tanzania baada ya kuishi Indonesia kwa zaidi ya
miaka nane na atafanya nini?
“Kuna mambo
mengi sana ya kufanya, lakini tunaweza kuzungumza kwanza masuala ya soka na
baadaye, nitawaeleza mambo yatakavyokuwa na kipi ambacho nimepanga kukifanya,”
anasema Masatu katika mahojiano yake ya kwanza na gazeti la Championi ikiwa ni
siku moja tu baada ya kutua nchini.
Kuna mambo
mengi sana kuhusiana na Simba, lakini umbo lake na namna alivyoweza kucheza na
kuwa beki bora lakini pia kuhusiana na fainali ya Kombe la Caf, mwaka 2003 kwa
kuwa Masatu alikuwa kati ya wachezaji walioelezwa kuhusika na hujuma.
Lakini
Masatu anaanza kuelezea kwa ufupi kuhusiana na maisha yake wakati akiwa Simba
na hadi alivyoondoka, mara ya mwisho aliingia katika mgogoro na kufikia hata
kutaka kumpiga kiongozi mmoja wa Simba.
“Simba
ndiyo ninayoipenda, nimecheza pale kwa moyo mmoja ingawa mpira wa Tanzania
kipindi kile ulikuwa na mambo mengi sana ambayo unaweza ukashangaa hata kama
ukiambiwa unaweza kukataa.
“Simba ni
timu kubwa, lakini ilifikia wakati tunasafiri kwa roli lakini wachezaji
walicheza bado kwa moyo na kutaka kushinda. Nakumbuka miaka michache kabla
sijaondoka Simba tulisafiri na basi kwenda Lindi.
“Ilikuwa ni
mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kariakoo Lindi. Tukiwa njiani basi liliharibika
mara kadhaa, ulikuwa usumbufu mkubwa na ikafikia wakati likakwama sehemu na
tukasukuma na kulitoa, safari ikaendelea.
“Lakini
tulipofika sehemu nyingine tena, gari likaharibika na kulikuwa na hofu huenda
tungechelewa hata kucheza mechi. Hivyo tukaomba msaada kwenye roli la mchanga
kutoka kampuni iliyokuwa inatengeneza barabara na tukalazimika kulipa ili
twende Lindi.
“Wale jamaa
wakawa tayari kutoa lile roli, lakini baadaye wakasisitiza ilikuwa ni lazima
kila mchezaji lazima alipe nauli ya shilingi elfu moja kwa kuwa hatukuwa mbali
sana kabla ya kufika Lindi. Wakati ule hatukuwa na fedha na hakukuwa na njia ya
kutuma.
“Mimi
niliwaambia viongozi kuwa nina fedha na waniahidi kunirudishia na mimi nitakachofanya
ni kutoa, wakakubali na nikafanya hivyo. Safari ikaendelea na tukafika Lindi
ambako nakumbuka tulicheza na kuifunga Kariakoo kwa mabao 2-1.
“Wakati huo
timu hiyo ilikuwa haifungiki pale Lindi, kwani hata ufunge bao vipi utaambiwa
ni offside, lakini sisi tulifanya kazi ya ziada na kuwafunga na hawakuwa na
ujanja kutokana na mabao yetu,” anasema Masatu.
“Pamoja na
ushindi huo, bado katiika kambi ya Simba kulitokea matatizo makubwa sana, hii
ilisababishwa na uamuzi wa uongozi kuwapa baadhi ya wachezaji nafasi ya
kusafiri na ndege wakati wengine tulipanda lori.
“Sisi
tukiwa kwenye basi na baadaye lori, kipa Mohammed Mwameja na Renatus Njohole
wao walikuja na ndege hadi pale. Hii iliwaudhi wachezaji wengi sana na
kusababisha zogo kubwa wakati wa kikao. Nilichofanya mimi ni kujaribu kuwapoza
wachezaji nikitumia neno la riziki ya mwenzo huwezi kuizuia.
“Ajabu
kiongozi mmoja, nakumbuka alikuwa anaitwa Kipukuswa, yeye aliendelea kunisakama
kwa maneno. Kweli roho iliniuma sana kwa kuwa nilikuwa nimetoa fedha yangu
kuhakikisha timu inafika lakini ukiachana na hivyo, bado nilijitahidi kusaidia
kuwapoza wachezaji wapunguze hasira, nikamvaa.”
“Wote
tulianguka chini, wakati huo sikujali tena kama kulikuwa na heshima. Maana
niliona kuna tatizo pia roho iliniuma kutokana na maneno ya kashfa ambayo
kiongozi huyo alikuwa anatoa mbele ya watu wote pale. Zogo kubwa likaibuka.”
BAADA ya
Masatu kupanda jazba na kumvaa Kipukuswa, hali ya amani ilipotea katika kambi
ya Simba. Je, nini kiliendelea? Kuna mtu alijitokeza kuwaamua au kuna mtu
aliumia katika ugomvi huo? Masatu ataendelea kusimulia likiwemo suala la fainali
ya Kombe la Caf mwaka 1993 ambayo yeye na wenzake walielezewa kupanga matokeo
kwa kushirikiana na mdhamini wakati huyo Azim Dewji ili Simba ifungwe na kukosa
kombe. Simulizi ya Masatu itaendelea keshokutwa IJUMAA, USIKOSE.








0 COMMENTS:
Post a Comment