*Kila moja itaondoka na Sh milioni 140
Uongozi wa kampuni ya Bakhresa inayomiliki klabu ya
Azam na Azam TV umemwaga dola milioni moja (zaidi ya Sh bilioni 1.6) ili kupata
haki ya udhamini wa Ligi Kuu Bara kama warushaji wa matangazo ya televisheni.
Kutokana na kumwaga fedha hizo, kampuni
hiyo kupitia kituo chake kipya cha televisheni yake ya Azam TV, kitakachoanza
kurusha matangazo hivi karibuni, kitapewa haki ya kuonyesha mechi zote za Ligi
Kuu Bara.
Kampuni hiyo iliyokuwa inapambana na
Supersport ya Afrika Kusini iliyokuwa tayari kutoa dola 500,000 imeihakikishia
bodi ya ligi hiyo kuwa iko tayari kutoa fedha hizo na kila klabu zikiwemo Yanga
na Simba zitapata Sh milioni 140 kila moja.
Pamoja na fedha hizo kutoka kwa wamiliki
hao wa Azam FC ambayo ndiyo wapinzani wakubwa wa Simba na Yanga, klabu hizo
kongwe zimesema zinataka kulipwa zaidi kwa kuwa ndiyo zenye mashabiki wengi.
Katika kikao kilichofanyika juzi,
kumezuka mjadala mkubwa huku Simba na YAnga zikisisitiza kwamba haitakuwa haki
zenyewe kupewa Sh milioni 140 sawa na klabu nyingine ambazo zina mtaji mdogo we
mashabiki.
“Lakini watu wa bodi ya ligi wameonyesha
kutokuwa waungwana maana wameendelea kulazimisha Simba na Yanga zilipwe sawa na
klabu hizo ndogo. Sisi tunaona hii si sahihi,” kilieleza chanzo cha uhakika.
Chanzo kingine kimeeleza, uamuzi huo wa
kampuni ya Bakhresa kupewa nafasi kulikuwa kunapingwa ‘kiana’ na watu wa klabu
hizo kubwa bila ya kujali inatoa fedha nyingi mara mbili ya SuperSport kwa
madai eti ni kubwa na wataonekana nchi nyingi.
Lakini wajumbe wengine walisisitiza
suala la fedha lipewe kipaumbele na fedha nyingi ndiyo zichukuliwe, hapo ndipo
kukaibuka suala la mvutano wa Yanga na Simba kutaka kupewa zaidi.
Taarifa zinaeleza tayari ufungaji wa
mitambo ya Azam TV inaendelea kwa kasi ya ‘kimondo’ na baada ya siku kadhaa
itaanza kazi huku ikitumia mitambo ya kisasa kabisa ikiwezekana kuliko
inayomilikiwa na kampuni nyingine za runinga nchini.








0 COMMENTS:
Post a Comment