OKWI AKITUMIKIA ESS... |
Na Saleh Ally
Taarifa zinaeleza kuwa klabu ya Simba
imemuuza kiungo wake nyota Emmanuel Okwi kwa klabu ya Etoile Du Sahel kwa dau
la dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 486).
Sh milioni 486 si fedha kidogo kwa Simba,
hakika unaweza kusema ni mpango mzuri kwa kuwa unaisaidia Simba kuingiza fedha
nyingi ambazo zitakuwa ni sehemu ya kusaidia maendeleo.
Kawaida moja ya biashara ambayo
inaziingizia klabu nyingi fedha barani Ulaya na kwingineko ambako mchezo wa soka
umeendelea ni kununua wachezaji kwa bei ya chini au kawaida, inawakuza na
kuwaendeleza halafu inawauza kwa bei juu.
Mfano mzuri ni Manchester United
ambayo ilimnunua Cristiano Ronaldo kutoka Sporting Lisbon ya Ureno akiwa kinda
kwa kiasi cha pauni milioni 12 na kumuuza kwa pauni milioni 80 kwa Real Madrid.
Utaona namna Manchester United
ilivyofaidika kutokana na uuzwaji wa mchezaji huyo, lakini hiyo ni sehemu tu ya
mfano kwa kuwa klabu nyingi zinafanya kwa kufaidika na mauzo ya wachezaji
kwenda klabu nyingine.
Katika biashara ya Simba na Etoile Du
Sahel kuna walakini mkubwa ambao hakika umekuwa ukiendelezwa bila ya mwanachama
hata mmoja kupata nafasi ya kuhoji udhaifu mkubwa kupindukia katika soka la
wakati huu.
Ilichofanya Simba ni biashara katika
mchezo wa soka ambayo ilikuwa ikifanyika miaka 20 au 30 iliyopita, si sasa.
Kufanya biashara kwa kusema imemuuza mchezaji, halafu isipate hata senti na
baada ya hapo ndiyo inasumbuka kumpata mnunuzi alipe deni ni kitu cha ajabu.
Simba wamemuuza Okwi kwa fedha nyingi,
halafu hadi leo haijapata hata senti moja. Vibaya zaidi imekuwa ikitumia fedha
kwenda Souness, kwa ajili ya kudai fedha zake.
‘Akili’ ya biashara lazima iwe
muongozo katika suala la uuzwaji wa wachezaji, Simba haijaenda na mfumo huo na
hata kama ikitokea ikalipwa fedha hizo, basi kuna mambo mengi na hasara itakuwa
imepata.
Mfano, fedha hazijapatikana katika
wakati mwafaka, najiuliza vipi Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alikubali
kufanya biashara hiyo hata bila ya ‘advance’. Na hasara zinazofuata kwa Simba
ni kama hivi.
Kwanza, tayari Simba imekosa mambo
lukuki na huenda ikaendelea kukosa katika kipindi hiki cha usajili kutokana na
kukosa fedha. Kama wangekuwa wamelipwa katika kipindi mwafaka, basi klabu hiyo
ingekuwa na nafasi nzuri ya kufanya usajili bora kwa ajili ya timu yake.
Lakini sasa Simba inahaha kutafuta
fedha kila sehemu, wakati mwingine imekuwa ikilazimika kutaka kutanguliza ‘mali
kauli’ kwa kuwa haina fedha, lakini Waarabu wa Tunisia wameendelea kuzikalia
fedha hizo kwa visingizio lukuki.
Inawezekana kama wanazo basi
wanazifanyia biashara, lakini kama hawana wanasubiri hadi hapo watakapomuuza
Okwi, ndiyo wakate kiasi kidogo na kuilipa Simba. Wao watakuwa wamefaidika na
klabu hiyo ya Msimbazi itakuwa imetumika kufanya biashara kubwa ya kuwafaidisha
Etoile Du Sahel.
Kingine ambacho Simba watakuwa
wameingia hasara, ni fedha za kwenda kufuatilia malipo yao Tunisia. Sijui kama
itakuwa imetoa klabu au mdau tu kajitolea lakini mwisho Katibu Mkuu, Evodius
Mtawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Pope walilazimika
kusafiri kwenda nchini humo.
Wazo la Mtawala na Hans Pope kusafiri
kwenda Tunisia ni zuri kwa vile wanalazimika kufanya hivyo ili kupata uhakika
wa mambo na huenda kulikuwa na mazungumzo yaliyopinda. Kwa kuwa Waarabu
wanajiweza kwa maneno mengi, basi ahadi imetolewa hadi Septemba.
Lakini bado Simba imekula hasara kwa
fedha za usafiri na malazi nchini Tunisia. Kitu ambacho kama biashara mwanzo
ingefanyika katika utaratibu unaotakiwa, basi Simba isingeingia katika hasara
na upotezaji wa muda kama unaoendelea sasa.
Papara katika biashara ni hasara,
lakini viongozi wa klabu wanapaswa kujifunza na ikiwezekana waache mambo yaende
kitaalamu kwa kuwa wanaruhusu vijana wasomi kufanya kazi kwenye klabu zao.
Basi vizuri wakapewa nafasi ya kutoa
maoni au kuendesha mambo kama hayo ambayo yatasaidia klabu kufanya biashara
zake kitaalamu zaidi na si kama hii ya Okwi ambayo inaonyesha huenda kukawa na
harufu ya Simba kutopata lolote kama Waarabu hao hawatalipwa.
Waarabu wanaweza wasilipe wasipomuuza
Okwi, wao hawatapata hasara yoyote, Simba itakuwa imepoteza fedha na muda,
ambayo ni hasara kubwa sana kwa mtu yeyote mwenye hesabu za kibiashara kwenda
kwenye mafanikio.
Inawezekana kabisa bado viongozi wa
Simba wanaona suala hilo kama kitu cha kawaida tu, hakiwaumizi sana lakini
hakuna ubishi lazima wajifunze kutokana na walichokifanya sasa kwani
kimechelesha mambo mengi na si vibaya kusema wameutumia muda vibaya.
FIN.
Sijui kama nakubaliana na mawazo yako. Maana mchezaji pia ana maamuzi yake, klabu ya kumnunua imepatikana mchezaji anataka kuondoka ukimkatalia mkataba uko ukingoni anaondoka bure. Wakati mwingine kila mtu anafikili anaweza kufanya kitu kuliko mwingine na akalaumu mwingine alipofikia lakini hii si mathematical problem ambayo jibu ni moja.
ReplyDelete